Monday 25 January 2016

ANAJUA NINI ANAFANYA

Mara nyingi siyo (mara chache) mume au mke hujikuta mwenzake ni msumbufu kwa kuuliza maswali ambayo hayana msingi kwa kuwa kinachoulizwa ni kile ambacho mume au mke huwa anafahamu namna ya kukifanya.
Nahisi bado hujanielewa naongea kitu gani labda nikupe mfano.
Siku moja Judy na mume wake Jerry waliamua kwenda kuwatembelea wazazi wa Jerry ambao wapo nje kidogo ya mji wanaoishi.
Hata hivyo baada ya kufika nyumbani kwa wazazi wao wakaambiwa kwamba wazazi wao nao walipanga kwenda kutembelea shamba.
Wote kwa pamoja yani Judy, Jerry, mama yake Jerry na baba yake Jerry wakapanda gari moja na kuanza safari ya kuelekea shamba.
Judy alikaa kiti cha mbele na baba yake Jerry (mkwe) ambaye ndo alikuwa dereva na Jerry alikaa kiti cha nyumba pamoja na mama yake.
Baada ya kusafiri kwa muda fulani Jerry akahisi baba yake anaenda au kuelekea njia ambayo si yenyewe hivyo akamnong’oneza mama yake kwamba baba yake anaenda njia ambayo si yenyewe
(aliamini kwa kumwambia mama yake basi mama yake ataropoka maneno yasiyopimika kumsema baba yake kwa kitendo cha kuendesha gari kwenda njia ambayo si sahihi).
Cha ajabu mama yake akamjibu Jerry kwamba “Baba yako anajua anachokifanya” kitu ambacho kilimfanya Jerry ajiulize kwani angekuwa ni yeye anayepotea na kuelekea mahali siko mke wake angemsema kwa fujo kama kawekewa vuvuzela mdomoni.
Ni kweli baba alipotea njia hata hivyo baada ya muda akakumbuka kwamba amekosea hivyo akageuza gari na kuelekea kule ambako ni sahihi.
(alikuwa anajua anachokifanya)
Walipofika shamba baba yake aliiweka kofia yake juu ya kiti na baada ya muda akaamua kukaa na akawa kasahau kwamba anaikalia kofia na kuikunja kunja; ndipo Jerry akamwambia mama yake
“Unamuona baba anakalia kofia na kuikunja si mwambie anakalia kofia yake?”
mama yake akamjibu Jerry kwamba
“ Baba yako anajua kile anakifanya”
jibu ambalo pia lilimfanya Jerry afikirie upya kuhusiana na mahusiano yake na mke wake hasa suala la kukosoana vitu vidogo vidogo kama hivi.
Inawezekana umemwambia mume wako anatakiwa kupaka rangi nyumba na kila siku unarudiarudia kumsema ukiamini kwa kumpigia kelele basi ataanya kile unasema, Mumeo anajua kile anakifanya ndiyo maana pamoja na kumsema nyumba bado haijapakwa rangi!
Inawezekana kila siku unamwambia mke wako anatakiwa kuhakikisha drawer za makabati zinafungwa kila akifungua hata hivyo kila siku unazikuta zipo wazi, ukweli ni kwamba mke wako anajua kile anakifanya.
Ni kweli inawezekana umeshamwambia mpenzi wako akufanyie kitu Fulani na ni muda sasa umepita na bado hajatimiza au hajafanya, umeamua kumsema kila siku ili afanye au kutimiza ahadi yake, hata hivyo ukweli ni kwamba yeye ni mtu mzima na anajua kila anakifanya.
Kumbuka kuwa kwenye ndoa ni kuwa mtu mzima na mtu mzima hapigiwi kelele kama mtoto kwani kila mtu mzima anajua anachokifanya na hakuna kitu mwanaume hapendi kama mwanamke ambaye kila wakati ni kukosoa na kusema sema tu na kumuweka kundi moja na watoto;
Ukweli ni kwamba mume wako anajua anachokifanya pia mke wako anajua anachokifanya.
Wengi tumegundua hii siri hatupigishani kelele kwani nikimwambia mke wangu leo nitaosha dishes zote au nitakusaidia kufua nguo hana haja ya kuniliuza au kunikazania utafanya saa ngapi hiyo kazi badala yake anatakiwa kurelax na kuenjoy maisha kwani mume wake ninajua ninachokifanya na ninafahamu nitafanya wakati gani.
Usiumize kichwa chako, anajua anachofanya!

No comments:

Post a Comment