Sunday 22 March 2015

TAMAA YA KIMWILI INAVYOCHANGIA WAPENZI KUSALITIANA.

Kwanza na mshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijaalia afya njema Lakini pia niwashukuru wapenzi wasomaji wa safu hii ambao tuliweza kuwasiliana na kushauriana hili na lile katika tasnia hii adhimu ya mapenzi.  Nawakaribisha tena!

Labda kwa wale wasiofahamu niwaambie tu kwamba, dhana ya mapenzi ina wigo mpana sana na ndiyo maana hutasikia hata siku moja ‘tumepumzika’ kuyazungumzia. Hata hivyo, tunachofanya siku zote ni kukumbushana kwa yale tunayoyafahamu na kushauriana pale tunapohisi wengi hufanya makosa.

Baada ya kusema hayo, niende sasa kwenye mada yangu. Hakuna kitu kinachoumiza katika uhusiano wa kimapenzi kama kusikia mpenzi wako anatembea na mtu mwingine tena ambaye huenda unamfahamu, inauma kuliko maelezo. Ambao wamewahi kusalitiwa wanajua.

Ndiyo maana katika makala zangu nyingi huko nyuma nimekuwa nikieleza kwamba, unapobaini mpenzi wako ana uhusiano wa siri wa kimapenzi na mtu mwingine, muache haraka bila kujali maumivu utakayoyapata.

Nasema muache kwa sababu, kama utaamua kumsamehe na kukubali kuwa shetani kampitia, tarajia kuendelea kusalitiwa na kuumizwa zaidi.

Kwa kifupi kasi ya kusalitiana kwa wapenzi imekuwa ikiongezeka kila kukicha kiasi kwamba unapoingia katika uhusiano wa kimapenzi unahisi kama unaingia kwenye matatizo makubwa. Hii ni kwa sababu watu sio waaminifu kabisa kwa wapenzi wao.

Unaweza kuwa na mpenzi wako ambaye kila mnapoonana anakueleza kuwa, anakupenda, anakujali, hawezi kukusaliti na atakuwa na wewe katika shida na raha. Lakini huyo huyo usishangae siku moja ukamkuta yuko na mtu mwingine. Swali la kujiuliza ni kwamba, kwa nini wapenzi wanasalitiana?

Zipo sababu nyingi sana zinazowasukuma baadhi ya watu kudiriki kuwaumiza wenzao kwa kuchepuka nje ya uhusiano wao. Hata hivyo, leo nataka kuzungumzia namna tamaa ya fedha na ya kimwili vinavyochangia katika hili.

Kwa wale ambao wako kweye ndoa wakati mwingine, hasa wanawake wasipopatiwa mahitaji yao muhimu na akatokea jamaa na kumhakikishia kumpatia kila anachotaka, wanakubali mara moja bila kujua kwamba wao ni wake za watu ama wapenzi wa watu na kujikuta wanajenga mazoea.

Wengine wanapatiwa kila kitu na waume zao lakini sasa kinachotokea ni tamaa za kimwili tu ambazo zinawasumbua na kujikuta wanatafuta waume wengine huku wakidai kuwa, wanatafuta ladha tofauti.

Hili si kwa wanawake tu hata wanaume pia, unaweza kumkuta ana mwanamke bomba tu mwenye kila kigezo, lakini bado anakuwa na tamaa za kutafuta kimwana mwingine nje.

Mimi nadhani kuna kila sababu ya kila mmoja kujitambua na kuitambua thamani yake. Wewe kama ni mke wa mtu, ridhika na hali aliyonayo mumeo, fedha isikufanye ukamsaliti mtu ambaye ulimuahidi kumtunzia penzi lake.

Vivyo hivyo kwa mwanaume, ridhika na penzi unalolipata kutoka kwa mkeo/mpenzi wako. Mademu wa nje hawana maana kwako zaidi ya kukuingiza katika matatizo.

Kwa kifupi ni kwamba kusalitiana kwa wanandoa kumekuwa kukitokea kutokana na kuwepo kwa mazingira fulani ambayo baadhi yao wamekuwa wakishindwa kujizuia nayo hivyo kujikuta wanatoka nje ya uhusiano.

Ila sasa nalazimika kwa nguvu zote kuwashauri wale walio katika uhusiano wa kimapenzi, namaanisha wapenzi wa kawaida, wachumba ama wanandoa, tusiwe na tamaa za kijinga na kufikia hatua ya kuwasaliti wapenzi wetu.

Hivi unajisikiaje unapomvulia nguo mtu ambaye wala hana ‘future’ na wewe eti kwa sababu ya fedha? Hivi na wewe ukifanyiwa hivyo na mpenzi wako utajisikiaje? Elewa maumivu utakayoyapata pale utakaposikia mpenzi wako ana uhusiano na fulani ni hayo hayo atakayoyasikia mwenza wako.

Kuwa muaminifu, ridhika na unachokipata kmwake, muoneshe mapenzi ya dhati naye atafanya vivyo hivyo na kujikuta mnayafurahia maisha yenu.

Saturday 21 March 2015

BADO MAPENZI YANAKUTESA?..

NIANZE kwa kumshukuru muumba wa Mbingu na nchi, kwa rehema na fadhila anazonifanyia katika maisha yangu ya kila siku, ama kwa hakika ni Mungu mwenye upendo. Ahsante baba.

Natumanini hamjambo na kama unasumbuliwa na jambo lolote, iwe kiafya au kiuchumi naomba usikate tamaa kwani matatizo ni sehemu ya maisha, jambo la muhimu ni kumuomba Mungu na kujaribu kutafuta suluhu ya tatizo hilo.

Baada ya kusema hayo, basi tuingie moja kwa moja kwenye mada yetu kama inavyojieleza hapo juu.
Ni wazi kwamba mapenzi yanachukua nafasi kubwa sana katika maisha ya binadamu, na ipo dhahiri kwamba mapenzi yanaweza kuleta furaha maishani mwako lakini wakati huohuo yanaweza kuleta maumivu, mateso na karaha.

Watu wengi sana bado wanalizwa na mapenzi na hii ni kwa sababu hawafuati kanuni sahihi ya mapenzi, ndiyo, mapenzi yana kanuni zake.

Kwa bahati mbaya kabisa, kwa sasa mapenzi yamegeuzwa na kuwa kama kitu cha kujaribu au kufanyia biashara na ndiyo maana yanawatesa wengi. Lakini ni kwanini mapenzi  yaendelee kututesa?  au ni kwa sababu hatujui maana halisi ya mapenzi? Hebu tuyaangalie mapenzi kwa jicho la tatu.

MAPENZI NI NINI?
Katika hali ya kawaida, mapenzi hayaelezeki kuwa ni nini. Ni vigumu sana mtu kukueleza maana ya mapenzi ndiyo maana kila mtu ana uelewa tofauti juu ya suala hilo.

Mtaalamu mmoja wa masuala ya mapenzi Davis Kurt kutoka Colombia, aliwahi kuyaelezea mapenzi ndani ya kitabu chake cha More About Love, ambapo alisema; ‘Love is natural feelings, which take place from the deepest part of your heart upon somebody or something else’ akimaanisha kuwa mapenzi ni hisia za asili ambazo huchukua nafasi kutoka sehemu ya ndani kabisa ya moyo juu ya mtu au kitu chochote. Tena bila kuwa na visingizio au masharti ya aina yoyote.

HISIA NI NINI?
Huu  ni msukumo wa vichochezi katika homoni za  ndani ya mwili ambazo hutokea kutokana na  mazingira husika.
Lakini huwa tofauti kati ya mtu na mtu na ndiyo maana watu hutofautiana madaraja ya kupenda.

Mfano halisi ni kwamba, utakuta mtu anapenda sana wanawake weupe, lakini mwingine hataki hata kuwaona.
 Lakini mapenzi siyo mawazo au uamuzi wa mtu, bali mapenzi ni hisia ambazo hutokea pasipo uamuzi wa mtu.

Kutokana na hali hiyo, utasikia mtu akisema ‘sijui nimempendea nini huyu mwanaume’ ni kweli yeye hajaamua lakini hisia zimefanya awe hivyo.

USIRUHUSU  MAPENZI YAKUTESE
Kwa nini mapenzi yakuumize? Unakosea wapi, kwanini ukataliwe kila mara? Haya ni baadhi ya maswali ya kujiuliza kuhusu mateso ya mapenzi.

Kamwe katika maisha yako usiruhusu mapenzi yakutese, najua yawezekana kila mpenzi unayempata haudumu naye, wewe ni mtu wa kulia kila siku, hujawahi kufurahia maisha hataa siku moja, jipange upya.

Thamini na jali zaidi maisha yako kwanza, fikiria kipi ni bora kati ya mapenzi na maisha yako, ni kipi kilitangulia? Kama maisha ndiyo yalitangulia  kwa nini usijijenge kwanza kimaisha ndipo mengine yafuate?

Hata kama unateswa na mtu unayempenda kwa dhati, hata kama ni mzuri kushinda malaika, kwani bila yeye maisha hayaendi? Si kweli na kama unaweza kuishi bila yeye kwa nini akutese namna hiyo?

Mpenzi msomaji wangu, hakuna kitu kinachouma kama mapenzi endapo utakosea kanauni zake, ukaruhusu moyo wote kuelekea huko, hakika yatakutesa.

Tuesday 17 March 2015

JINSI YA KUDUMISHA UHUSIANO WA MBALI.

Siku zote mapenzi huyapa maisha thamani lakini wapo ambao hujikuta kwa namna moja ama nyingine wanatengana na wapenzi wao kwa sababu tu ya mihangaiko ya kila siku ya kujitafutia riziki. Masomo na wakati mwingine utengano huwa ni matokeo ya wapendanao kuishi sehemu tofauti.
Umbali hulifanya penzi baina ya wapendanao kuteteleka kama wapendanao hawatafanya kazi za ziada kuhakikisha wanaziba mianya yote itakayosababisha usaliti kama sio kuachana kabisa.
Hata hivyo, mapenzi ya mbali huna ni vigumu kuteteleka endapo tu wapendanao wanamapenzi ya dhati na kutamani kuwa pamoja kila wakati na mmoja wapo kuamua kujitoa muhanga kwa kuamia anakoishi ama anakofanyia kazi laazizi na mwandani wake.
Pamoja na hayo yote bado umbali hauwezi kuwa ni tatizo kubwa sana la kutetelesha uhusiano wako na mpenzi wako. Mnaweza kudumisha mapenzi yenu ya mbali endapo
utafanya haya:-

1.MAWASILIANO MARA KWA MARA.

Mawasiliano ni nguzo muhimu sana baina ya wapendanao, humfanya kila mtu kuhisi uwepo wa mwenzi wake hata kama atakuwa mbali naye.
Hivyo, kama una mpenzi wako aliye mbali nawe hakikisha unakuwa naye karibu kwa kumtumia ama sms, email, kadi au simu.
Aidha, pindi mnapowasiliana hakikisha humkwazi mwenzako kwa namna yoyote ile, kwani kuna watu wengi wanatabia ya kudharau baadhi ya mambo kutokana na kutingwa na shughuli kadha wa kadha, naomba nikuweke wazi kuwa hata kama umebanwa vipi pindi mpenzi wako aliye mbali anapokutumia ujumbe kwenye simu yako basi usisite kumjibu katika muda muafaka na siyo kuuchuna hadi ulalamikiwe!

2.HESHIMU HISIA ZAKO:

Mapenzi ya kweli yametawaliwa na hisia kali ambazo ndizo huwafanya wapendanao kufikishana kwenye mambo fulani kwani pasipo hisia hata uwe na ujuzi au utundu wakutosha hutapata raha ya mapenzi.
Kama kweli unampenda kwa dhati mwenza wako na mmetengana kutokana na sababu za kimasomo ama kazi kwa hakika utakuwa tayari kumtunzia penzi lake hadi mtakapokutana tena.
Uaminifu pekee ndio utakaokufanya uwasiliane mara kwa mara na mwenza wako na kwenye uaminifu mapenzi hushamiri huku kila mmoja akimuonea wivu wa hapa na pale mwenzi wake (lakini sio ule wakubomoa!) Hivyo heshimu hisia zako kama kweli unampenda mwenzi wako kwa kumuonesha unampenda.

3.UMBALI ISIWE KIGEZO KUNYIMANA.

Mpe mwandani wako raha kamili kama ilivyokuwa awali mlipokuwa pamoja! Bila shaka unajiuliza inawezekanaje? Hili linawezekana kwa kutumia njia yoyote ya mawasiliano. Mfano kama nyote mna simu jiandae vya kutosha nikiwa na maana uhakikishe upo sehemu ambayo utakuwa huru kuongea ama kufanya chochote
Kitakachokufanya uhisi raha isiyo na kifani na kukufikisha kwenye kilele cha mlima kilimanjaro bila kutarajia.
Bila shaka kila mtu anamfahamu vema mpenzi wake na hasa nini hupenda kufanyiwa ili awezekufika safari yake na kama ndivyo basi hakikisha unafanya mambo yote ambayo ukimfanyia mwenzi wako pindi mnapokuwa kwenye mambo fulani hupagawa.
Nilshawahi kueleza namna ya kujigijigi kupitia kwenye simu.

KWANINI WAPENZI HUGOMBANA?

Mara kwa mara nimeshuhudia viugomvi vya wapenzi au wanandoa....
" Tunapendana sana lakini tunaviugomvi vya mara kwa mara. Sijui ni kwa nini hii hali, tunajaribu kuondokana nayo lakini tunashindwa"

Katika makala hii ninajaribu kuonyesha baadhi ya sababu zinzaofanya wapenzi au wanandoa wengi kugombana mara kwa mara ingawa viugomvi hivi havimaanishi kwamba hawapendani na sio kwamba kugombana huku mara kwa mara wako tayari kuachana.

SABABU

1. PALE MPENZI MMOJA ANAPOSHINDWA KUFANYA YALE YALIYOTARAJIWA NA MWINGINE.

Kila mmoja wetu ana picha akilini mwake inayomwenyesha ni jinsi gani mpenzi au mwenza bora anatakiwa awe, picha hii yamkini imechoreka akilini mwetu tangia utotoni. Bila kudhamiria mara nyingi tunajikuta tunaanza kulinganisha kile tulichokuwa nacho akilini na kile kilicho dhahiri kinachotokea. Katika mapenzi kwa sasa. Mara nyingi wakati tunapojikuta tunagombana ni kutokana na utofauti wa vile mpenzi wako anavyofanya na vile ulivyomtarajia akilini mwako awe.

Uhalisi unatokea unapokuwa tofauti na tuliyotarajia, hisia zetu zina umizwa, chuki inaamka, maumivu yanaibuka na hivyo hasira na ugomvi huja. Hasira hapa hutumika kama njia ya kumlazimisha mpenzi au mwenza wako kukaribia au kujaribu kuwa kama yule mpenzi bora uliyekuwa unamuwaza akilini mwako. Ingawa mara nyingine pamoja na hasira hizi yawezekana tusione hata chembe moja ya badiliko. Wapenzi wengi husihi miaka mingi hususani kwenye ndoa nakuwa ndani ya chuki za aina hii na walioshindwa kukidhi haja za kila mmoja.

2. PALE UNAPOKUWA NA TOFAUTI KALI KATIKA MISIMAMO YENU

Misimamo hii ni zile imani au vitu tunavyoviamini na vinavyotusaidia kuendesha maisha yetu ya kila siku. Kila mmoja wetu anavimisimamo anavyosimamia kila siku maishani. Vitu ambavyo tunaviamini na tunavipa uzito tofauti vitu hivyo. Mfano, Kama msimamo au imani ya mmoja wenu ni kihifadhi fedha na mwingine ni kuzitumia lazima tofauti baina yenu itakuwa kubwa, kwa sababu wakati mmoja anajitutumua kutafuta fedha na kuziweka kwa maendeleo mwingine anajitahidi kuzitumbua kwa matumizi yasiyo na msingi, hapa lazima moto uwake baina ya wawili hawa.

Kama mmoja anapenda kujinyenyekeza na anaamini kuwa mume au mpenzi wa kiume anatakiwa kunyenyekewa, na wakati mwingine anaamini katika usawa wa jinsia, lazima hapa ugomvi usiishe. Ugomvi unakuwa lazima katika wapenzi wa aina hii maana kila mmoja anaamini kitu ambacho ni cha tofauti kabisa na mwingine, na kila mmoja anajaribu kuhimiza kila anachoamini kifanyike.

3. PALE TUNAPOTOFAUTIANA NAMNA TUNAVYOTAFSIRI MAHITAJI YETU YA KIHISIA

Wengi wetu kama sio wote hupenda vitu vitatu toka kwa wengine, Upendo, Kutambuliwa na Heshima. Ingawa tunajitahidi kutunza mahitaji yote matatu lakini moja lina yazidi mengine, hii ni hitaji la upendo au penzi toka kwa yule unayempenda. Tatizo linakuja kwamba penzi halishikiki kwa hiyo ni ngumu kulipa picha fulani, ndiyo maana ninapoouliza mwanaume yeyote, unajuaje kwamba mkeo anakupenda swali hili linakuwa gumu sana kujibu. Wengine hutokea haswa pale tupotofautiana kutafsiri jinsi ya kuelezea penzi. Wengine wanataka walione penzi kwa macho, waone wanavyopendwa, wengine wanataka wasikie jinsi wanavyopendwa na wengine wanataka wahisi vile unavyompenda, sasa kama wewe unaona kupenda kwa kweli lazima mtu aone penzi kwa macho, wakati yeye anaamini ni lazima asikie hilo penzi masikioni mwake basi mtatofautiana sana na hamtaisha kubishana.

Ndio maana wako wapenzi wnaoona wamependwa na kuthaminiwa pale tu wanapopewa vitu vya thamani au kufanyiwa suprize, wakati wengine hutaka wasikie maneno kama " nakupenda" I love u" "Umependeza" ndio wajue wanapendwa, hata kama hujapewa kitu chochote. Wapo ambao wanataka kuguswa, kukumbatiwa na wapenzi wao na katika hali hii watahakikisha kuwa wanapendwa, Jiulize sasa, wewe penzi unalitazamaje Nini kifanyike ili uone kama unapendwa.

3.PALE AMBAPO UJUMBE ULIOKUSUDIWA KUTUMWA SIVYO ANAVYOKOLEWA

Magomvi mengi tena makali hutokea baina ya wapenzi wengi pale ambapo mmoja anatuma ujumbe fulani au kusema kitu fulani na yule anayepokea msikilizaji anahisi kama anaeelewa na kuanza kutenda kumbe anatenda tofauti, pasipo kuuliza aeleweshwe anafanya kile alicho au anachokiwaza akilini mwake kuwa ndicho sahihi kwa jinsi alivyokitafsiri.

Mfano, mpenzi wa kiume anasema "njoo hapa" Mpenzi wakike mara anajibu " kwani nimefanya nini"? najibu hivi kutokana na kuhisi kuwa sauti hii iliyomwita ni yashari, kumbe sivyo awazavyo mpenzi wa kiume. Najua jinsi alivyouta yaweza maanisha anahasira na wewe lakini pia yaweza maanisha amekasirishwa na kitu au vitu vingine. Chakufanya hapa. jifunze kuhakikisha kile ulichosikia au unachohisi umekielewa kabla hajarukia katika kutafsiri isivyo sahihi.


Tuesday 10 March 2015

TAMBUA UTAMU WA MAPENZI NA JINSI GANI YA KUULINDA.

 Kuna sababu za msingi kabisa kuelezea mambo ya kuzingatia ili kutambua vitu vitakavyokufanya ufurahie utamu wa ndoa yako. Kuishi na mke au mume sii kitu rahisi kama ambavyo watu wengi ambao hawako katika ndoa hufikiria. Hivi ni vipengere baadhi tu, wanandoa na wampenzi wanapaswa kuvitambua;

Kwanza kabisa ni kwambie kwamba utamu wa mapenzi si lazima ufanye tendo la ndoa ama ngono, kuna mambo kibao ambayo moyo wa binadamu ukiyakosa huweza kukonda kama muathirika wa magonjwa hatari ya mwili.

*UPENDO KUTOKA KWA YULE UMPENDAE.

hili ndilo jambo kubwa la kwanza katika afya ya moyo ulio katika dimbwi la mapenzi.

Hakuna kitu kitamu kama kupendwa na ukapenda pia, kitendo hiki hufunga macho yote ya vishawishi vya dunia hii ya kidigitali. Usilazimishe upendo kwa mtu ambae unaonekana kuwa wewe tu ndiye unaye mjali wakati yeye hana habari na wewe. Ndio maana ukitaka kuingia katika ndoa lazima umtafute mtu unayempenda na anayekupenda ili muishi katika maisha yasiyo ya kushawishika kufuata matamanio mengine nje ya ndoa.

*AMANI.

Watu wengi wana wanaume na wanawake warembo, lakini hawafurahii mapenzi kwasababu hawana amani ndani ya nyumba. Utafurahia utamu wa mahusiano ya ndoa endapo utakuwa na moyo uliopondeka mbele za Mwenyezi Mungu, yani kuvumiliana katika changamoto za maisha.

Wapo watu wao ni maarufu kwa kuharibu mahusiano ya watu "tofauti na ndugu yako wa karibu" hakuna mtu anayefurahia kukuona unamwanamke mrembo ndani ya nyumba au mwanaume mtanashati ndani ya nyumba, na kwambia hili, jifunze kutunza siri za uzuri wa mkeo au mmeo. Kunawatu wanavitaka vitu hivi sana hata kwa gharama yoyote ile na popote vitakapopatikana vitanakuwa halali yao.

Kama mpenzi wako anakupa penzi tamu na la kistaarabu, basi haina haja ya kumueleza rafiki yako maana hujui yeye anakosa nini katika mahusiano yake na mwenzi wake. Pesa ni silaha kubwa sana katika mapenzi haya ya kizazi cha digitali, pesa zimekuwa na ushawishi mkubwa sana katika mapenzi hivyo unapaswa kuwa msiri katika mambo yako ya chumbani.

Cha msingi zaidi, hakuna mtu anayefurahi kusalitiwa katika mapenzi, kila mtu anatamani kummiriki mwenzi wake asipate wazo la kutoka nje ya mahusiano. Tunajua kabisa dunia hii kila siku tunakutana na wasichana warembo kabisa na pia tunakutana na wanaume watanashati si kidogo, lakini kitu cha msingi ni kuyashinda majaribu yote ili kuilinda amani ya mahusiano yako.

Thursday 5 March 2015

MSAMAHA,NENO DOGO LENYE THAMANI KUBWA KATIKA MAPENZI.

Hebu jiulize unaelewaje juu ya msamaha? Umewahi kuomba, kuombwa au kusamehe? Kuna faida zozote za kuomba msamaha? Mada hii itakupa majibu ya mswali haya na utaona thamani kubwa ya msamaha.

Kwanza kabisa msamaha ni nini? Ni neno dogo, maarufu sana katika jamii yetu ambalo kwa hakika hutumiwa na watu wengi, lakini lina maana kubwa zaidi ya litumiwavyo.

Ni kawaida sana kumsikia mtu akisema: “Nisamehe bwana, nisamehe mshkaji wangu...” kirahisi tu, mtu anazungumza.

Hata hivyo, Wanasaikolojia wanasema asilimia 60 ya wanaoomba msamaha huwa hawaombi kutoka mioyoni mwao.

Matokeo hayo yalipatikana kutokana na utafiti uliofanywa ukiwahusisha ndugu na wapenzi waliokoseana. Aidha, inaelezwa kwamba, asilimia 30 ya wanaokubali kusamehe, hawasamehi moja kwa moja kutoka mioyoni mwao.

Yaani anakubali usoni lakini moyoni kuna kitu tofauti na kinachoonekana machoni mwa mhusika.

Msamaha sahihi ni ule ambao muombaji anapoomba kusamehewa anakuwa anaamaanisha anachozungumza, ni rahisi kusoma hilo katika mboni za macho yake, lakini pia hata yule anayesamehe ni vema kama atakubali kusamehe kwa moyo wake. Huo ndiyo msamaha wa kweli rafiki zangu.

KWANINI TUNAOMBA KUSAMEHEWA?
Kikubwa zaidi kinachotafutwa katika kuomba msamaha ni amani ya moyo! Unapoomba msamaha unakuwa na amani moyoni mwako baada ya kuwa huru kutokana na kosa ulilomfanyia mtu.

Unaweza kukosana na ndugu, rafiki au mpenzi wako, ni hali ya kawaida ambayo haishangazi sana. Ngoja nikupe mfano mmoja; Mwaka 2007, katika mkutano wa mwisho wa mwaka wa wafanyakazi kazini kwetu, bosi wangu aliwahi kusema:
“Naruhusu watu wakosee, lakini hairuhusiwi kurudia kosa.

Kukosea ni mwanzo wa kujifunza, kwahiyo kosea ili ujifunze, ukishajua hutakosea tena.”

Baadhi ya watu hawakuelewa sentesi hiyo tata, lakini ilikuwa na maana kubwa sana kwa wafanyakazi.

Vivyo hivyo, hata katika uhusiano wa kimapenzi, inaruhusiwa kabisa kukosea ili uweze kujifunza kutokana na makosa. Kwa maneno mengine ni kwamba, unapokosea na ukajua kwamba umekosea, omba msamaha ili uweze kuwa na amani ya moyo.

KWANINI TUSAMEHE?
Maana ya kipengele kichopita, haitofautiani sana na hii, unaposewa ni wazi kwamba unakuwa na kinyongo moyoni mwako, sasa unapoombwa msamaha ni kama ulikuwa na mzigo mzito ambao sasa unautua na kupumzika!

Kamwe usikatae kusamehe, lakini kama mwombaji anaonekana anaigiza, mweleze ukweli, kuwa pamoja na kwamba umemsamehe umegundua kwamba anaomba msamaha kwa ajili ya kukuridhisha tu.

Hii itamfanya kwanza, ajione siyo mjanja kama alivyofikiria, kwamba uwezo wako wa akili ni mkubwa, umegundua kilichokuwa akilini mwake, hakika ni lazima atabadilisha hisia zake na pengine ataamua kurudia kukuomba msamaha kwa kumaanisha.

Vipi kwa anayekosea kila mara?
Wapo ambao wanashindwa kuwasamehe wenzi wao kwa sababu eti wanakosea kila mara, huu ni upotoshaji! Huna sababu ya kuhesabu makosa, ingawa mkosaji ana deni la ufahamu kuwa kukosea mara moja inaruhusiwa maana anajifunza, lakini kurudia kwa mara nyingine inahesabika kama ni makusudi.

Wewe samehe kadri uombwavyo msamaha, maana hata maandiko yanasema: “Samehe mara saba, sabini.” Maandiko hayaishii hapo, bado yanasisitiza:

“Utusamehe makosa yetu kama tunavyowasamehe waliotukosea.” Bado yanasema: “Amri kubwa nawaachieni, pendaneni.” Hivi ni baadhi ya vipengele vinavyopatikana katika sehemu za maandiko matakatifu.

Lakini kubwa zaidi ambalo unapaswa kujiuliza, ni mara ngapi umekuwa ukimkosea
Mungu na kumuomba msamaha? Na mara zote hizo, amekusamehe au bado amekuwa na kinyongo na wewe? Ukweli ni kwamba, Mungu wetu hahesabu makosa, sasa kwanini wewe unahesabu? Samehe usamehewe.

Jifunze kitu kipya...
Unapokosea na kuomba msamaha, fahamu kwamba unakuwa umemkwaza sana mwenzi wako, lakini pia katika ufahamu huo, lazima uwe makini sana na kutokurudia makosa kwa
mara nyingine.

Jifunze upya, uahidi moyo wako kutokukosea tena, kisha anza upya ukifanya mambo mapya kuliko kuzidi kurudia makosa. Kosea kosa lingine, siyo lile uliloomba msamaha awali. Pia ni vema ukajizoesha kuomba msamaha, neno hilo lisiwe gumu kwako, liwe sehemu ya maisha yako.

Omba msamaha kila unapokosea, lakini pia wewe ambaye unaombwa msamaha, kubali kusamehe. Jizoeshe, kusamehe kama sehemu ya maisha yako, utaona mafanikio
katika maisha yako.

ZINGATIO LA MWISHO
Ni imani yangu kwamba mada hii imekupa mwanga mpya katika maisha yako ya
kimapenzi. Sasa unaweza kuishi salama, hata kama utakosewa au kwa bahati mbaya kukosea. Silaha yako kubwa ni kuomba msamaha na kukubali kusamehe.

Hata katika uhusiano wako au ndoa, samahani ni neno lenye hadhi kubwa sana.
Litumie kukufanya mwenye furaha siku zote za maisha yako.

Naamini mada hii imekuwa dawa tosha katika uhusiano wako.

Wednesday 4 March 2015

UNAMPENDA NA UNAHITAJI NDOA KUTOKA KWAKE?...SIMA HAPA UFAHAMU JINSI YA KUFANYA

Karibu tena tujadiliane kuhusu mada ya leo kama inavyojieleza; unampenda na unataka kumuoa lakini hujui pa kuanzia, unapaswa kufanya nini?

Maendeleo ya teknolojia yamebadilisha mambo mengi katika maisha yetu ya kila siku. Zamani ilikuwa kama kuna mwanamke au mwanaume unampenda, basi lazima uhangaike sana mpaka utakapopata nafasi ya kuzungumza naye, na kama huna ujasiri wa kumtongoza ana kwa ana basi ndiyo umemkosa.
Siku hizi mambo yamebadilika sana. Ukitokea kumpenda mtu fulani kama kweli nia yako ni kuingia naye kwenye ndoa na siyo kukidhi matamanio ya siku moja, zipo mbinu nyingi zinazoweza kukurahishia kazi yako. Kuna simu za mikononi, kuna mitandao ya kijamii na njia chungu nzima hivyo huna haja ya kuendelea kuumia na upweke.


Kumbuka kuwa penzi bora ni lile ambalo wawili huanza kwa kuwa marafiki, ni makosa kukurupuka kumtongoza mtu kwenye simu au kwenye mitandao ya kijamii bila kumvuta kwanza karibu yako na kumfanya kuwa rafiki yako.

Hatua ya kwanza, kama nilivyosema hapo juu ni kujitahidi kujenga ukaribu naye. Kama unadhani ni vigumu kwa wewe na yeye kukutana ana kwa ana, unaweza kutafuta namba yake ya simu. Ukishapata namba ya simu ya huyo umpendaye, tafuta muda ambao utakuwa umetulia kisha mpigie na jitambulishe.
Mweleze kwamba umempigia simu kumjulia hali, kama akikuuliza mahali ulikoipata namba yake, unaweza kumjibu vyovyote lakini inashauriwa kuwa siyo vizuri kumtajia aliyekupa namba yake kwa sababu unaweza kuwagombanisha.
Usiwe na papara, mtakie siku njema na endelea na shughuli zako nyingine. Unaweza pia kuendelea kumtumia meseji za kawaida (siyo za mapenzi), ukimjulia hali, ukimuuliza kama ameshakula au amekula chakula gani, anafanya nini kwa muda huo na vitu anavyovipenda sambamba na vile asivyovipenda.

Endelea hivyo kwa muda, siri kubwa ambayo huijui ni kwamba watu wengi, hasa wanawake huwa wanapenda kujua kuwa mtu fulani anamjali kwa kumuuliza mambo mbalimbali yanayohusu maisha yake ya kawaida. Jitahidi kuwa mcheshi lakini usizidishe masihara. Ukishafanikiwa kumvuta karibu yako na kumfanya aamini kwamba huwa unamfikiria mara kwa mara, sasa unaweza kupiga hatua moja mbele kwa kufanya yafuatayo:

Tumia sauti ya utulivu yenye hisia ndani yake, utazidi kumvuta karibu yako. Usipende kuzungumza kwa sauti ya juu au kupayuka au kupiga simu ukiwa kwenye kelele. Akipokea tu simu yako, mjulie hali yake kisha msifie kidogo kuhusu sauti yake na namna anavyozungumza.
Msimulie kidogo kuhusu siku yako inavyokwenda, tumia maneno machache lakini yatakayomfanya asiboreke kukusikiliza. Ifanye stori yako iwe ya kuvutia kwa kutumia maneno matamu yatakayomfurahisha na kumfanya aache kila anachokifanya na kukusikiliza.

Badili mazungumzo, muulize kama anajua kwamba yeye ni mzuri sana na hujawahi kukutana na mtu anayevutia kama yeye. Kama wewe ni mwanaume na unayezungumza naye ni mwanamke, utakuwa katika nafasi nzuri ya ‘kum-win’ kwa sababu wanawake wengi wanapenda sana kusifiwa.

Akiwa amekolea na sifa unazommwagia, mweleze kwamba unavutiwa naye na unatamani kuwa na mpenzi anayefanana naye. Zungumza naye kwamba atakapokubali kuwa na wewe, utamtunza na kumlea kama malkia, mweleze malengo yako ya baadaye katika uhusiano wenu endapo atakukubalia.

Usimpe nafasi ya kukwambia kama amekubali au amekataa bali hitimisha mazungumzo yenu kwa kumtakia siku njema au kazi njema. Bila shaka utamuacha akiwa na shauku kubwa ya kuendelea kusikiliza ‘mistari’ yako.
Endelea kuwasiliana naye kwa mambo ya kawaida huku ukimpima kama yale uliyomwambia anayachukuliaje. Kama naye amekupenda, utaanza kuona mabadiliko kuanzia meseji atakazokuwa anakutumia