Thursday 5 March 2015

MSAMAHA,NENO DOGO LENYE THAMANI KUBWA KATIKA MAPENZI.

Hebu jiulize unaelewaje juu ya msamaha? Umewahi kuomba, kuombwa au kusamehe? Kuna faida zozote za kuomba msamaha? Mada hii itakupa majibu ya mswali haya na utaona thamani kubwa ya msamaha.

Kwanza kabisa msamaha ni nini? Ni neno dogo, maarufu sana katika jamii yetu ambalo kwa hakika hutumiwa na watu wengi, lakini lina maana kubwa zaidi ya litumiwavyo.

Ni kawaida sana kumsikia mtu akisema: “Nisamehe bwana, nisamehe mshkaji wangu...” kirahisi tu, mtu anazungumza.

Hata hivyo, Wanasaikolojia wanasema asilimia 60 ya wanaoomba msamaha huwa hawaombi kutoka mioyoni mwao.

Matokeo hayo yalipatikana kutokana na utafiti uliofanywa ukiwahusisha ndugu na wapenzi waliokoseana. Aidha, inaelezwa kwamba, asilimia 30 ya wanaokubali kusamehe, hawasamehi moja kwa moja kutoka mioyoni mwao.

Yaani anakubali usoni lakini moyoni kuna kitu tofauti na kinachoonekana machoni mwa mhusika.

Msamaha sahihi ni ule ambao muombaji anapoomba kusamehewa anakuwa anaamaanisha anachozungumza, ni rahisi kusoma hilo katika mboni za macho yake, lakini pia hata yule anayesamehe ni vema kama atakubali kusamehe kwa moyo wake. Huo ndiyo msamaha wa kweli rafiki zangu.

KWANINI TUNAOMBA KUSAMEHEWA?
Kikubwa zaidi kinachotafutwa katika kuomba msamaha ni amani ya moyo! Unapoomba msamaha unakuwa na amani moyoni mwako baada ya kuwa huru kutokana na kosa ulilomfanyia mtu.

Unaweza kukosana na ndugu, rafiki au mpenzi wako, ni hali ya kawaida ambayo haishangazi sana. Ngoja nikupe mfano mmoja; Mwaka 2007, katika mkutano wa mwisho wa mwaka wa wafanyakazi kazini kwetu, bosi wangu aliwahi kusema:
“Naruhusu watu wakosee, lakini hairuhusiwi kurudia kosa.

Kukosea ni mwanzo wa kujifunza, kwahiyo kosea ili ujifunze, ukishajua hutakosea tena.”

Baadhi ya watu hawakuelewa sentesi hiyo tata, lakini ilikuwa na maana kubwa sana kwa wafanyakazi.

Vivyo hivyo, hata katika uhusiano wa kimapenzi, inaruhusiwa kabisa kukosea ili uweze kujifunza kutokana na makosa. Kwa maneno mengine ni kwamba, unapokosea na ukajua kwamba umekosea, omba msamaha ili uweze kuwa na amani ya moyo.

KWANINI TUSAMEHE?
Maana ya kipengele kichopita, haitofautiani sana na hii, unaposewa ni wazi kwamba unakuwa na kinyongo moyoni mwako, sasa unapoombwa msamaha ni kama ulikuwa na mzigo mzito ambao sasa unautua na kupumzika!

Kamwe usikatae kusamehe, lakini kama mwombaji anaonekana anaigiza, mweleze ukweli, kuwa pamoja na kwamba umemsamehe umegundua kwamba anaomba msamaha kwa ajili ya kukuridhisha tu.

Hii itamfanya kwanza, ajione siyo mjanja kama alivyofikiria, kwamba uwezo wako wa akili ni mkubwa, umegundua kilichokuwa akilini mwake, hakika ni lazima atabadilisha hisia zake na pengine ataamua kurudia kukuomba msamaha kwa kumaanisha.

Vipi kwa anayekosea kila mara?
Wapo ambao wanashindwa kuwasamehe wenzi wao kwa sababu eti wanakosea kila mara, huu ni upotoshaji! Huna sababu ya kuhesabu makosa, ingawa mkosaji ana deni la ufahamu kuwa kukosea mara moja inaruhusiwa maana anajifunza, lakini kurudia kwa mara nyingine inahesabika kama ni makusudi.

Wewe samehe kadri uombwavyo msamaha, maana hata maandiko yanasema: “Samehe mara saba, sabini.” Maandiko hayaishii hapo, bado yanasisitiza:

“Utusamehe makosa yetu kama tunavyowasamehe waliotukosea.” Bado yanasema: “Amri kubwa nawaachieni, pendaneni.” Hivi ni baadhi ya vipengele vinavyopatikana katika sehemu za maandiko matakatifu.

Lakini kubwa zaidi ambalo unapaswa kujiuliza, ni mara ngapi umekuwa ukimkosea
Mungu na kumuomba msamaha? Na mara zote hizo, amekusamehe au bado amekuwa na kinyongo na wewe? Ukweli ni kwamba, Mungu wetu hahesabu makosa, sasa kwanini wewe unahesabu? Samehe usamehewe.

Jifunze kitu kipya...
Unapokosea na kuomba msamaha, fahamu kwamba unakuwa umemkwaza sana mwenzi wako, lakini pia katika ufahamu huo, lazima uwe makini sana na kutokurudia makosa kwa
mara nyingine.

Jifunze upya, uahidi moyo wako kutokukosea tena, kisha anza upya ukifanya mambo mapya kuliko kuzidi kurudia makosa. Kosea kosa lingine, siyo lile uliloomba msamaha awali. Pia ni vema ukajizoesha kuomba msamaha, neno hilo lisiwe gumu kwako, liwe sehemu ya maisha yako.

Omba msamaha kila unapokosea, lakini pia wewe ambaye unaombwa msamaha, kubali kusamehe. Jizoeshe, kusamehe kama sehemu ya maisha yako, utaona mafanikio
katika maisha yako.

ZINGATIO LA MWISHO
Ni imani yangu kwamba mada hii imekupa mwanga mpya katika maisha yako ya
kimapenzi. Sasa unaweza kuishi salama, hata kama utakosewa au kwa bahati mbaya kukosea. Silaha yako kubwa ni kuomba msamaha na kukubali kusamehe.

Hata katika uhusiano wako au ndoa, samahani ni neno lenye hadhi kubwa sana.
Litumie kukufanya mwenye furaha siku zote za maisha yako.

Naamini mada hii imekuwa dawa tosha katika uhusiano wako.

1 comment: