Sunday 22 March 2015

TAMAA YA KIMWILI INAVYOCHANGIA WAPENZI KUSALITIANA.

Kwanza na mshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijaalia afya njema Lakini pia niwashukuru wapenzi wasomaji wa safu hii ambao tuliweza kuwasiliana na kushauriana hili na lile katika tasnia hii adhimu ya mapenzi.  Nawakaribisha tena!

Labda kwa wale wasiofahamu niwaambie tu kwamba, dhana ya mapenzi ina wigo mpana sana na ndiyo maana hutasikia hata siku moja ‘tumepumzika’ kuyazungumzia. Hata hivyo, tunachofanya siku zote ni kukumbushana kwa yale tunayoyafahamu na kushauriana pale tunapohisi wengi hufanya makosa.

Baada ya kusema hayo, niende sasa kwenye mada yangu. Hakuna kitu kinachoumiza katika uhusiano wa kimapenzi kama kusikia mpenzi wako anatembea na mtu mwingine tena ambaye huenda unamfahamu, inauma kuliko maelezo. Ambao wamewahi kusalitiwa wanajua.

Ndiyo maana katika makala zangu nyingi huko nyuma nimekuwa nikieleza kwamba, unapobaini mpenzi wako ana uhusiano wa siri wa kimapenzi na mtu mwingine, muache haraka bila kujali maumivu utakayoyapata.

Nasema muache kwa sababu, kama utaamua kumsamehe na kukubali kuwa shetani kampitia, tarajia kuendelea kusalitiwa na kuumizwa zaidi.

Kwa kifupi kasi ya kusalitiana kwa wapenzi imekuwa ikiongezeka kila kukicha kiasi kwamba unapoingia katika uhusiano wa kimapenzi unahisi kama unaingia kwenye matatizo makubwa. Hii ni kwa sababu watu sio waaminifu kabisa kwa wapenzi wao.

Unaweza kuwa na mpenzi wako ambaye kila mnapoonana anakueleza kuwa, anakupenda, anakujali, hawezi kukusaliti na atakuwa na wewe katika shida na raha. Lakini huyo huyo usishangae siku moja ukamkuta yuko na mtu mwingine. Swali la kujiuliza ni kwamba, kwa nini wapenzi wanasalitiana?

Zipo sababu nyingi sana zinazowasukuma baadhi ya watu kudiriki kuwaumiza wenzao kwa kuchepuka nje ya uhusiano wao. Hata hivyo, leo nataka kuzungumzia namna tamaa ya fedha na ya kimwili vinavyochangia katika hili.

Kwa wale ambao wako kweye ndoa wakati mwingine, hasa wanawake wasipopatiwa mahitaji yao muhimu na akatokea jamaa na kumhakikishia kumpatia kila anachotaka, wanakubali mara moja bila kujua kwamba wao ni wake za watu ama wapenzi wa watu na kujikuta wanajenga mazoea.

Wengine wanapatiwa kila kitu na waume zao lakini sasa kinachotokea ni tamaa za kimwili tu ambazo zinawasumbua na kujikuta wanatafuta waume wengine huku wakidai kuwa, wanatafuta ladha tofauti.

Hili si kwa wanawake tu hata wanaume pia, unaweza kumkuta ana mwanamke bomba tu mwenye kila kigezo, lakini bado anakuwa na tamaa za kutafuta kimwana mwingine nje.

Mimi nadhani kuna kila sababu ya kila mmoja kujitambua na kuitambua thamani yake. Wewe kama ni mke wa mtu, ridhika na hali aliyonayo mumeo, fedha isikufanye ukamsaliti mtu ambaye ulimuahidi kumtunzia penzi lake.

Vivyo hivyo kwa mwanaume, ridhika na penzi unalolipata kutoka kwa mkeo/mpenzi wako. Mademu wa nje hawana maana kwako zaidi ya kukuingiza katika matatizo.

Kwa kifupi ni kwamba kusalitiana kwa wanandoa kumekuwa kukitokea kutokana na kuwepo kwa mazingira fulani ambayo baadhi yao wamekuwa wakishindwa kujizuia nayo hivyo kujikuta wanatoka nje ya uhusiano.

Ila sasa nalazimika kwa nguvu zote kuwashauri wale walio katika uhusiano wa kimapenzi, namaanisha wapenzi wa kawaida, wachumba ama wanandoa, tusiwe na tamaa za kijinga na kufikia hatua ya kuwasaliti wapenzi wetu.

Hivi unajisikiaje unapomvulia nguo mtu ambaye wala hana ‘future’ na wewe eti kwa sababu ya fedha? Hivi na wewe ukifanyiwa hivyo na mpenzi wako utajisikiaje? Elewa maumivu utakayoyapata pale utakaposikia mpenzi wako ana uhusiano na fulani ni hayo hayo atakayoyasikia mwenza wako.

Kuwa muaminifu, ridhika na unachokipata kmwake, muoneshe mapenzi ya dhati naye atafanya vivyo hivyo na kujikuta mnayafurahia maisha yenu.

No comments:

Post a Comment