Wednesday 15 July 2015

MAMBO YA KUEPUKA WAKATI WA MIGOGORO YA NDOA.

Hapo kila mtu kivyake, Kila mtu mbabe, kila mtu anajiona hana kosa, hakuna kuongea, hakuna kugusana hata unywele; Ndoa ina raha yake hata mkosane vipi bado mnalala pamoja, hata hivyo kwa nini msijadili pamoja na kupata jibu then muendelee na kujirusha kama kawaida.

Kila mahusiano ya ndoa hukumbwa na migogoro ya hapa na pale, inaweza kuwa wakati wa raha au wakati wa shida kwa kuwa ni binadamu migogoro huja yenyewe hadi kifo kitakapowatenganisha.
Kitu cha msingi ni kufahamu kwa nini kuna mgogoro au tatizo, na umesababishwa na nini na ni njia ipi itumike kutatua hilo tatizo na zaidi kusameheana kwa pamoja na kusahau.

Tafiti nyingi zinaonesha kwamba mawasiliano mazuri kwenye mahusiano ya ndoa huongeza;
Utamu wa mahaba,
Kuaminiana na
Kusaidiana,
Na mawasiliano ovyo huweza kuharibu kabisa uimara wa ndoa na kujenga kutokuaminiana na zaidi ndoa kwenda ndivyo sivyo.
Kuna mambo ambayo tunapofanya kwenye ndoa huwa tunaona kama vile tunatatua tatizo kumbe ni kinyume chake, hebu angalia wewe ni lipi kati ya yafuatayo umekuwa unayafanya na pia kama unaweza badilisha huo mtazamo au njia ili kuimarisha mahusiano yako na huyo umpendaye.

Moja ya mwanandoa kukwepa tatizo au mgogoro:

Badala ya kujadili tatizo lililopo kuna watu huamua kubaki kimya tu kana kwamba tatizo litayeyuka lenyewe kama barafu.
Na wakati huohuo kutokana na tatizo au mgogoro mtu anakuwa na mawazo kiasi kwamba unajua kuna jambo linamsuta kwenye mawazo na moyo wake.
Hadi tatizo au mgogoro ukue sana ndipo kwa hasira mtu anapasuka.
Kuogopa eti tutabishana sana isiwe sababu ya kuacha tatizo liwe linakaa tu, ni jambo la busara kuelezena ukweli na kulimaliza tatizo na yule ambaye amekosea akubali na mwenzake amusamehe kwani hakuna aliye mkamilifu asilimia mia, bali kwa udhaifu wetu tunasaidiana na kukamilishana hivyo kuwa wazi na kuliezeza tatizo au mgogoro na hatimaye kupata suluhisho ndiyo dawa kamili si kubaki kimya.
Pia wapo wanandoa ambao tatizo likitokea anakataa katakata kabisa kuongea na anaweza kusema hilo tutaongea kesho na kesho anakwambia kesho, then kesho hadi inakuwa mgogoro mzito.

Kujilinda:

Badala ya kufungua moyo na kumuelewa mwenzako wewe unakataa kusababisha tatizo mbaya zaidi unakwepa kwamba kuhusika katika hilo tatizo au mgogoro.
Hapo badala ya kutatua tatizo unaongeza zaidi kwani mwenzio kwanza atajisikia kwamba hujamsikiliza na pia umemdharau kwa kujiona wewe huna kosa.
Matokeo yake tatizo au mgogoro utaendelea kukua na kufukuta.
Kitu cha msingi hata kama unahisi huhusiki basi msikilize mwenzako na jaribu kuangalia umehusika vipi kusababisha mgogoro au tatizo lenyewe kuliko kukimbilia kujilinda kwamba hijahusika.
Wanaume (siyo wote) hapa ndo panatukamata sana huwa tunajiona huwa hatukosei na wakati mwingine hata kosa au tatizo likitokea, sisi tunaona si kosa wala tatizo.
Wanawake ni watu wa hisia zaidi (emotional) na sisi tupo logical.
Inaweza kuwa kwako mwanaume si tatizo ila kwa mwanamke ni tatizo hivyo msikilize na angalia wewe umehusika vipi na zaidi shiriki ili kupata suluhisho na uhakikishe kila mmoja ameridhika.

Kudhani ni kawaida yake:

Kuna wakati tatizo au mgogoro ukitokea, wapo ambao huanza na sentensi kama zifuatazo,
“Kila siku upo hivihivi”
au
"siku zote huwa hunisikilizi”
au
“Hiyo ni kawaida yako”
au
“Nilijua tu utasema hivyo”
Usilete mambo ya nyuma kueleza kwa mwenzio tatizo au mgogoro uliopo, badala ya kutatua tatizo unaliongeza zaidi.
Kitu cha msingi mpe mwenzako nafasi aeleze jambo na pia husiku katika kuangalia chanzo cha tatizo ni nini siyo kurukia na kutoa hitimisho hata bila kujua jambo zima lipoje kisa unakumbukumbu ya makosa yake ya nyuma.
Mwenye kujenga ndoa ni wewe na mwenye kuibomoa ni wewe, usione watu wanadumu na ndoa zao, kitu cha msingi wanakuwa makini kusikiliza na kuhusika katika kutatua matatizo kwa kushirikiana bila kujali matatizo au makosa yaliyopita.

Kujiona mkamilifu
Kwa kuwa wewe ni binadamu hata kama umesoma au upo smart sana kwenye ndoa kuna siku unakosea tu, na pia ukubali kukosolewa na kukubali kukosa ili usamehewe pia.
Wapo wanandoa ambao yeye siku zote yupo sahihi na mwenzake ndo mkosaji.

Kumsoma mwenzako:

Wapo wanandoa hujiona wao wanafahamu na kujua kutafsiri hata mambo ambayo mwenzake anawaza au anafanya.
Au ukifanya kitu anatafsiri anavyojua yeye.
Kwa mfano; ukichelewa nyumbani kurudi, anakwambia humjali au humpendi, Usipimpigia simu anasema humjali au humpendi, au ukikataa tendo la ndoa kwa sababu unajisikia umechoka anasema humjali.
Kitu cha msingi fahamu tatizo au sababu ni nini kwa kuongea na mhusika ndipo utoe maamuzi yako.

Kutokusikiliza:

Kuna wanandoa ambao mwenzake akianza kumueleza tatizo hata kabla hajamaliza anadakia na kuanza kubwabwaja anachojua yeye, badala ya kusikiliza point zilizomo kwenye hicho anaambiwa.
Ni vizuri unapoongea na mke au mume na kama amekuomba aongee na wewe baada ya kuona kuna tatizo ni vizuri kumsikiliza kwa makini kuliko hata unavyomsikiliza bosi wako kazini, kwani usipomsikiliza mke au mume na mgogoro ukawepo hata kazini unaweza kufanya madudu.

Kulaumiana:

Kuna watu ambao style yao ni kwamba tatizo likitokea tu yeye ni kulalamika na kulaumu mwenzake, bila hata kuchunguza vizuri chanzo na kiini cha tatizo.
Hujiona kukiri udhaifu ni kujishusha sana mbele ya mwenzake, kama ni mwanaume atalalamika na kujiosha kwamba yeye hahusiki (ingawa anajua amehusika ila mfume dume) na badala yake kesho anakuletea zawadi ili yaishe, huko siyo kutatua tatizo bali ni ujanja tu.
Tathmini hali ya tatizo kwa pamoja na shirikiana kumaliza tatizo.
Tumia tatizo au mgogoro kama nafasi (stepping stone) ya kuweza kutengeneza ndoa kufikia viwango vya juu zaidi.

Kuonekana mshindi;

Kama kila tatizo likitokea wewe ndo unataka kuonekana upo sahihi na mshindi ujue unadhoofisha mahusiano ya ndoa yako.
Kila mara tunapokutana na matatizo lengo ni kutaka kushirikiana kutatua na zaidi kufikia muafaka huku kila mmoja akimheshimu mwenzake.
Unapong’angania au kulazimisha kwamba mwenzako ndo amekosea hapo unaumiza hisia zake na kuumiza hisia za mpenzi wako ni kitu kibaya sana.

Kumfikiria vibaya mwenzako:

Wapo wanandoa ambao udhaifu wa mwenzake katika jambo fulani anaupa kibandiko (label) cha kudumu.
Kwa mfano, mwanaume ambaye akivua nguo chumbani anaziweka mahali popote; mke wake anafikia uamuzi kwamba huyu ni mzembe na mvivu na anaachana naye kujadili na kumsaidia kuongea naye kuhusu hiyo tabia.
Au mwana mke ambaye kila tatizo likitokea anamuomba mume wajadili; na mume ana chukulia kwamba ni mtu msumbufu sana kila jambo kujadili.
Kitu cha msingi kila binadamu ana tabia imara na dhaifu; hivyo wewe ni mtu pekee ambaye unaweza kumsaidia kuondoa hizo tabia dhaifu kwa upendo na kushirikiana.

No comments:

Post a Comment