Tuesday 16 December 2014

UTENDEE HAKI MOYO WAKO.

HEBU jiulize kwa nafasi yako hapo ulipo, unautendea haki moyo wako? Mpenzi uliyenaye unampenda au unajilazimisha kuwa naye?

Elewa kuwa mapenzi ni sehemu ya maisha yetu na kwa hakika maisha yetu hayawezi kukamilika bila kuwepo mapenzi.Ninapozungumza juu ya mapenzi namaanisha yale yanayotoka moyoni mwa mtu mmoja kwenda kwa mwingine.

Mapenzi ya dhati ambayo hayachagui fedha wala dhiki, ambayo hayatofautishi sherehe na huzuni, maradhi na faraja!. Moyo wako ukubali kwa dhati na kwa hali zote kama nilivyoeleza hapo juu.

Mapenzi hukamilika baada ya wawili kuwa na hisia sawa za mapenzi. Amini kama upo katika uhusiano na mpenzi ambaye hakupendi, yaani wewe peke yako ndiyo unayempenda, wewe ni mtumwa wa mapenzi! Kama ndivyo, kwa nini uwe mtumwa?

Unadhani hakuna mwingine ambaye anaweza kukupenda kwa mapenzi ya dhati na penzi hilo likawa kwa pande zote mbili tofauti na ilivyo sasa?

Inawezekana huna sababu ya kulazimisha penzi kwa mtu ambaye hakupendi! Mapenzi ni nguzo ya maisha yetu, kama ukifanikiwa kumpata mpenzi ambaye atakupenda na wewe ukampenda ni wazi kuwa maisha yako yatakuwa yenye furaha na hakika utafurahia sana maisha yako na huyo mwandani wako!

Mapenzi yapo hivyo na kama ukijaribu kuyabadilisha utaumia mwenyewe! Wakati mwingine unaweza ukapendwa na mpenzi ambaye hujampenda, unadhani kuna ulazima wa wewe kulazimisha kumpenda?

Moyo wako umeshazungumza na wewe, umekuweka wazi kuwa hauna mapenzi ya dhati kwa mtu huyo, kwa nini ujilazimishe? Tatizo hili mara nyingi huwa kwa wanawake zaidi!

Anatokea mwanaume anampenda sana, anapomtongoza anajikuta kuwa hampendi, anachokifanya ni kumwambia kuwa atamjibu baadaye! Lengo la kumwambia hivyo ni kwa ajili ya kujipanga na kufikiria. Hakuna mapenzi ya aina hiyo, Hisia hazifikiriwi! Kama mtu unampenda, unapomuona tu siku ya kwanza, moyo wako hutetemeka juu yake na hutamani uambiwe kitu fulani na huyo aliyeuteka moyo wako ghafla.

Hii ina maana kuwa atakapokuambia kuwa anakupenda, huwezi kusubiri zaidi, hutakuwa na kitu cha kusubiri, ni nafasi uliyokuwa ukiisubiria kwa hamu kubwa sana.

Hapo sasa lazima utamkaribisha! Huo ndiyo ukweli. Moyo wako unapaswa kuwa muamuzi wa mwisho na siyo kuingia kwenye uhusiano ukiwa huna mapenzi kwa nia ya kujifunza kupenda.


Posted via Blogaway

No comments:

Post a Comment