Thursday 7 May 2015

CHUKI KWA MPENZI WAKO WA ZAMANI HAINA FAIDA..UNAPOTEZA MUDA..

MAPENZI yana siri kubwa. Kila mmoja ana ugonjwa wake wa kupenda. Wengine wanawapenda wapenzi warefu, lakini kuna kundi ambalo huchanganyikiwa zaidi kwa wafupi. Pamoja na mchanganuo huo, kuachwa inauma hata kama anayekutosa hukuwa na mapenzi naye.

Ile dhana tu ya kuachwa ndiyo hutesa watu. Kuna dhana kwamba anayeacha mara nyingi hujiona mshindi dhidi ya aliyemuacha. Na hiyo ndiyo sababu ya wengi kuumia wanapofungiwa milango ya kukatisha uhusiano ambao pengine hata hawakuwa na maslahi nao.

Watu wanaingia kwenye mapenzi na baadaye wanatengana. Wapo wanaobaki na amani, lakini wengine wanaendelea kuishi katikati ya chuki.
Husalimiani na mwenzi wako wa zamani, mbaya zaidi pengine huyo uliye na uhasama (bifu) naye, mmefanikiwa kupata mtoto pamoja. Usiangalie moyo wako, zingatia ukuaji wa mwanao.

Hapa nifafanue kitu kimoja kwamba sifundishi watu kuwakaribia wenzi wao wa zamani, la hasha! Nashauri kutowekeana uadui kwa sababu hauna maana.
Mtaalamu mmoja wa saikolojia ameandika: “Moja kati ya njia rahisi ya kupoteza muda wako ni kumchukia mwenzi wako wa zamani.” Binafsi nakubali, kwa nini ujenge bifu na mtu aliye nje ya mzunguko wako wa maisha?

Naweza kuelewa kwamba kumchukia mtu ambaye hayupo tena kwenye mzunguko wa maisha yako, ni kama hatua ya kujipa maumivu ya moyo au huzuni isiyo na sababu.
Ukimchukia mwenzi wako wa zamani, maana yake unaendelea kumhifadhi kwenye moyo wako. Aghalabu utakumbuka mabaya yake lakini kuna vipindi vichache ambavyo mazuri yake yatakujia.

Endapo kuna mambo yake mazuri yatakuja kwenye ubongo wako, yatakutesa. Utakumbuka namna alivyokujenga kimahaba, si ajabu utamkumbuka tena na kuanza kuhisi kumkosa.
Njia rahisi ni kuhakikisha moyo wako unakuwa mweupe. Unaachana na kumbukumbu zote. Funga ukurasa wa zamani na ufungue mpya. Maisha yaendelee, Siku Hazigandi, wazungu wanasema life goes on.

Hatari kubwa katika chuki yako kwa mwenzi wako ni kuendelea kujipa maumivu ambayo si ajabu yatakuja kukusababishia ujione wewe bila yeye ni sawa na kukabiliana na kifo.
Kinyume cha mapenzi siyo chuki. Ni kutojali (kupotezea). Yaani unapokosana na mwenzi wako, usianze bifu, badala yake anza kumpotezea na usimjali kwa chochote.

Tafsiri nzuri ya kumchukia mwenzi wako wa zamani maana yake bado unampenda na bado unahitaji kuendelea naye.
Watu wengi wanatangaza kuachana na wenzi wao lakini wanaendelea kudumisha ukaribu bila sababu za msingi, ingawa kuna uwezekano mkubwa mioyo yao ndiyo inayowatuma.

Kwa taarifa ni kwamba kitendo cha kuendelea kuwa karibu na mwenzi wako wa zamani, maana yake unakaribisha fursa ya wewe na yeye ya ama kukumbushia au kurejea upya kwenye mapenzi.
Tafsiri nyingine ni kwamba ile chuki ambayo wewe unakuwa nayo inatokana na ukweli kwamba unahitaji aje kwako lakini unaona wazi kuwa hana mpango nawe hata kidogo.

Ukweli ni kwamba wewe mwenyewe utajiona umebeba mzigo wa usumbufu kumchukia mpenzi wako wa zamani ambaye huna ukaribu naye.
Kwa mwanamke, nafasi kubwa kwake katika maisha yake, mara mnapoachana, atatengana na wewe kwa sababu maalumu. Ukionesha nia ya kuendelea naye, atarejea kwako kwa ari zaidi.

Unatakiwa kwenda mbele kukabiliana na matukio mapya ikiwa unaumizwa na machungu ya kuachana na mwenzi wako.

No comments:

Post a Comment