Saturday 7 May 2016

TIBA YA MAMA MKWE.


Hapo zamani za kale kulikuwa na Binti aitwaye Lily aliolewa, yeye na mume wake wakaenda kuishi kwa mama wa mume wake yaani mama mkwe.
Kwa muda mfupi tu walioishi Lily aligundua kwamba yeye na mama mkwe hawaendani kabisa, walitofautiana kwa kila kitu na Lily alikasirishwa sana na tabia za mama mkwe wake kwani mama mkwe alikuwa anamlaumu muda wote.

Siku zilipitia, wiki zikapita na miezi ikapita kila siku Lily na mama mkwe ni kuzozana na kushambuliana, kibaya zaidi ni kwamba kutokana na traditions ilimpasa Lily kumpigia goti kila lile ambalo mama mkwe alihitaji afanye na ukweli hali mbaya ya mahusiano kati ya Lily na mama mkwe ilimfanya hata mume wake Lily kujisikia vibaya sana.

Mwisho Lily hakuweza tena kuvumilia tabia mbaya na utawala wa mama mkwe hivyo akaamua kufanya kitu, hivyo akafunga safari kwa rafiki wa baba yake ambaye alikuwa anauza dawa za kienyeji.
Alipofika kwa huyo Mzee akamweleza yote anayokutana nayo na kwamba anaomba msaada kama anaweza kumpa sumu ili aweze kumuua yule mama mkwe na kuondokana na lile tatizo milele.

Mzee akafikiria kwa muda na mwisho akamwambia Lily atamsaidia kulimaliza tatizo lake ingawa Lily alitakiwa kusikiliza kwa makini na kutii kile ataambiwa akafanye.

Na Lily naye kwa furaha akajibu kwamba nitafanya chochote utaniambia nifanye.
Ndipo Mzee akaingia ndani na kutoka na mfuko uliosheheni dawa na akaanza kumpa maelezo Lily
"Huwezi kutumia sumu ya haraka kumuua mama mkwe wako kwani kila mmoja atakutilia mashaka wewe hivyo nimekupa kiasi cha kutosha cha dawa (herbs) ambayo itatumika kidogo kidogo na kujenga sumu ya kutosha na hatimaye kumaliza.
Hivyo kila siku tengeneza mlo safi na weka dawa kidogo kwenye hicho chakula.
Sasa, ili kila mtu asikutilie mashaka wewe hasa akifa lazima uwe makini sana kujifanya rafiki kwake, usibishane naye na kubali chochote anakwambia na umuhudumie kama vile ni malkia, si unajua ipo siku atapotea kabisa”.

Lily alikuwa na furaha ya ajabu, akamshukuru mzee na akaenda nyumbani kuanza shughuli ya kumuua mama mkwe wake.

Miezi ikapita, wiki zikapita na siku zikapita, Lily aliendelea kumpa mama mkwe chakula chenye ile sumu na alikuwa anakumbuka sana jinsi Mzee alivyokuwa amemweleza jinsi ya kuepuka kutiliwa mashaka, hivyo aliweza kujizua hasira zake na alimtii mama mkwe kwa kila kitu na alimhudumia kama mama yake mzazi (malkia)

Baada ya miezi sita, nyumba nzima ilibadilika baada ya Lily kuweza kuzishinda hasira zake kwa mama mkwe na kumtii na wakajikuta hawagombani tena na hawakuweza kuzozana au kubishana kwa miezi sita mfululizo na wakajikuta wanaelewana na kuishi vizuri.
Pia mtazamo wa mama mkwe nao ulibadilika na alianza kumpenda Lily kama binti yake mwenyewe na akawa anawasimulia rafiki zake mwenyewe kwamba Lily alikuwa ni binti mzuri mwenye tabia njema ambaye hakuna mama mkwe duniani anaweza kumpata. Lily na mama mkwe wakawa ni kama mama na binti yake.

Pia mume wa Lily alikuwa na furaha ya ajabu alipoona kile kinatokea katika familia.
Ndipo Lily akarudi kwa mzee kuomba msaada tena, akamwambia mzee,
“Tafadhari nisaidie jinsi ya kuiondoa ile sumu isimuue mama mkwe kwani amebadilika na amekuwa mwanamke mwema sana kwangu na ninampenda kama mama yangu mzazi na sitapenda afe kwa sababu ya sumu niliyompa”.

Mzee akawa anatabasamu huku anatikisa kichwa.
“Lily huna haja kuwa na mashaka au kuogopa, sikukupa sumu yoyote, dawa niliyokupa ilikuwa ni vitamins kwa ajili ya kuimarisha afya. Sumu kubwa iliyokuwepo ilikuwa kichwani mwako (mind) na mtazamo wako kuhusu mama mkwe na hiyo sumu yote imesafishwa na upendo ambayo umeutoa kwake”.

Je, mdau wangu umegundua kwamba jinsi unavyowahudumia wengine ndivyo na wao watakavyokuhudumia wewe.


Inawezekana ni kweli unasuguana sana na mama mkwe au mume wako au mke wako au mpenzi wako na tatizo kubwa ni mtazamo wako kuhusu yeye na ungeamua kumpenda na kumhudumia kama malkia au mfalme mambo yangebadilika.

No comments:

Post a Comment