Thursday, 10 March 2016

NI UPI MTAZAMO WA NDOA YAKO.?

Moja ya tatizo la kawaida kwa ndoa za sasa ni mtazamo wa wanandoa kuamini kwamba ndoa yao haitafika popote au siku moja itashindikana au mmoja wa wanandoa kuwa na wazo kwamba siku moja ataondoka zake au wote kuwa na mtazamo kwamba siku moja nitaondoka na kuanza kivyangu upya.

Ukiwa na wazo la kushindwa ni hakika utashindwa vizuri sana kwani muda wote utakuwa unaangalia matatizo yote (negatives) ambayo yanakuwa alama kwamba sasa kushindikana kumeanza.
Yaani kwa kuwa una mawazo kwamba siku moja ndoa itashindwa basi akili yako hujipanga kusubiri dalili za kushindikana hata wewe mwenyewe kujua.

Wapo wanandoa wanaweza kusimama juu ya paa na kukiri kwamba ndoa zao ni za furaha hata hivyo ukichunguza kwa makini siri ya furaha yao si kwa sababu hawakutani na matatizo au shida au mambo magumu bali ni kwa sababu ya mtazamo wao kwamba wao ni mke na mume hadi kifo kitakapowatenganisha na zaidi sana wanajua sanaa ya kusuluhisha matatizo katika ndoa yao kwa kuanza na wao wenyewe kila mmoja kuamini kwamba anaweza kubadilika kwanza na kuleta mabadiliko na siyo kunyosheana vidole au kila mmoja kujiona yupo right all the time.

Inawezekana wewe unayesoma hapa sasa hivi ni mmoja ya wale ambao likitokea tatizo nyumbani na mumeo/mkeo basi ni kununa tu eti kwa kuwa siku moja utaondoka zako! Au kwa sababu una mipango yako kabambe na murua kabisa ya kumuacha mwenzio kwenye mataa hata hujafikiria watoto na huo uamuzi wako ambao ni kujifaraji tu kwani kuondoka si jibu la mambo yote bali ni njia nzuri ya kwenda kuanza kukutana na tatizo jipya na kubwa zaidi.

Kwani wewe ndo mtu wa kwanza kukutana na tatizo kama hilo kwenye ndoa?
Si kweli, badala ya kuchangamka na kupenda kwa moyo wako wote wewe unafikiria kuondoka au kudhani sasa mwisho wa ndoa umefika.

Eti tupo tofauti sana hatuwezi kuishi pamoja tena! Kwani ni nini kilikuvutia hadi ukakubali kuoana naye? Eti siku hizi simpendi kabisa! Lini umeanza kutompenda? Si umeamua mwenyewe kutompenda kwani love is a choice, wewe mwenyewe umeamua kutompenda na kweli humpendi ukichagua kumpenda utampenda.

Eti mke wangu ni mchafu sana! Unataka kumuacha kwa sababu ni mchafu? Mbona wakati wa uchumba alikuwa mchafu na ulikuwa una ignore! Nani mchafu kama si wewe uliyechumbia mwanamke mchafu, leo badala ya kutunza kilicho chako king’ae unataka kukimbia?

Unapoingia kwenye ndoa huku ukiwa na ufahamu au mtazamo kwamba ndoa ni hadi kifo kitakapowatenganisha hapo tayari umepiga hatua kubwa sana na mbali kukuhakikishia ndoa yako inadumu na kuwa ya furaha kwa sababu unakuwa tayari kukubali kurekebisha kila tofauti zinazojitokeza kwani unajua huyu ni mwenzi wangu na kuna umuhimu wa kuishi kwa furaha kila wakati.

Ukiingia kwenye ndoa huku unategemea kushindwa ni kweli utashindwa vizuri sana na ukitegemea kufanikiwa na kuwa na ndoa ya furaha ni kweli utakuwa na furaha na zaidi utajifunza njia ya kuwa na furaha na utakuwa moja ya wanandoa wenye furaha duniani.


posted from Bloggeroid

No comments:

Post a Comment