Sunday, 5 July 2015

RAHA YA KUWA NA MWENZA .

Watu hungia kwenye uhusiano ili kupata wa kushirikiana nao katika maisha,Kubwa watu husaka watakaowapa raha na si karaha.Kama unae mwenza halafu unampa shida,tambua kuwa haupo sawa na unapaswa kubadilika haraka.

Inashangaza kuna watu wapo katika uhusianolakini kila kukicha wanachokifanya ni kutiana hasira na mambo ĺmengine ya aina hiyo.Ukweli ni kwamba wanaofanya mambo hayo wanakosea.Maana ya kuwa na mpenzi ni kwamba awe mshirika wako mkubwa katika maisha,kwamba ukilia awe anauliza jamani unalia nini? Jamani nini kinakusumbua?.Siyo unakuwa na mtu unamringia.Hapo raha ya kuwa kwenye uhusiano inapungua.Maisha yanatuhitaji wakati mwingine kuwa kama watoto wadogo.Eeh ndugu yangu usione watu wanatembea mtaani,kuna wengine sehemu zingine wanapokuwa na wenzi wao wanakuwa kama watoto.Kuna ambao husema..tata kunywa uji..” na mtu analishwa hadi anashiba.Mpe raha mwenzi wako akufurahie.
Kuna watu kwa kweli kwa namna ambavyo wanaishi ni vile tu kwamba wao si Mungu,lakini wangekuwa na uwezo wangesema huyu mwanaume/mwanamke bora afe.Hata hivyo ni vizuri kwamba kunapokuwa na migogoro kuangalia namna ya kufanya ili kuondoa tatizo ambalo liko.
Katika maisha kukwazana ni suala la kawaida japo si vizuri.Cha msingi kunapokuwa na matatizo ni kukaa chini kuzungumza ili kuondoa tatizo lililoko,si vinginevyo.Mapenzi ni kama kilimo.Mtu anapokuwa na shamba mathalani la mahindi,majani yakiwa mengi watu si huwa wanapalilia ili mahindi yastawi? Na mapenzi hivyo hivyo,lazima yapaliliwe.Ni vizuri kuangalia namna ya kufanya ili kuhakikisha unaendelea kuwa na uhusiano imara na mtu ambaye uko naye.Matatizo ni sehemu ya maisha,kama ni kuachana,utaachana na wangapi ndugu yangu?
Hata kama labda mwenzi wako anaonekana kuwa na uhusiano na mwingine,katika maisha kilicho cha msingi ni kuangalia hasa sababu ya mtu kuwa wa ovyo ni nini? Kwa nini jana alikuwa mzuri,leo amekuwa mbaya?

Raha ya mapenzi au kupenda ni nini ikiwa kwenye uhusiano hakuna amani? Ni swali ambalo baadhi ya watu wamekuwa wakijiuliza.Uhusiano unapokuwa kwenye migogoro haina maana kwamba watu waachane,bali ni suala la kawaida,lililo la msingi kama watu wazima,kuyamaliza,mwendelee na maisha.

Raha ya mapenzi ni mapenzi.Hata kama mmekasirikiana,bado mnapaswa kuelewa kwamba hata babu zetu nao walikasirikiana,lakini walivumiliana.
Raha ya mapenzi ni kutoa na kupewa kitu roho inapenda pasipo kumuumiza mwenzio kwa namna yoyote.
Raha ya mapenzi ni kuvumiliana na kusameheana.kwa maana hiyo unapaswa kufahamu kuwa katika maisha ya mapenzi hua kuna migogoro,hivyo inapotokea unatakiwa kufahamu nini cha kufanya ili kuondoa kasoro hiyo.
Raha ya mapenzi ni kuwa na mtu ambaye moyo umeridhia kuwa naye,mnaheshimiana,kila mmoja anamjali mwingine na mnashirikiana kimawazo,kimali,kiushauri na maisha mengine kwa ujumla.Zaidi ni pale mnapokuwa wakweli,wawazi,wenye kusamehe na wenye malengo sahihi na yanayoeleweka na pande zote.
Raha ya mapenzi ni kumpenda anayekuoenda na vingine vitafuata.Hilo ni la msingi,unapaswa kumpenda mtu kutoka moyoni mwako,wala si kwa kushinikizwa kwa namna au sababu zozote.
Kwa mtazamo wangu raha ya mapenzi ni kumpata akupendaye kwa dhati na umpendaye kwa dhati katika shida na raha mkipeana mapenzi ya dhati.

No comments:

Post a Comment