Tuesday, 14 July 2015

HAWA NDIO WANAUME.

Je, Mwanamke huwa unatoa ushauri kwa mumeo baada ya kuombwa na yeye au unatoa tu kwa sababu unampenda?

Je, utajibiwa au mzee anaamua kula jiwe na kuumiza hisia zako?

Ilitokea siku moja John na Mkewe walikuwa wanaendesha gari lao kuelekea kwenye sherehe za harusi posta mpya jijini DSM.
Mzee John ndiye alikuwa anaendesha gari.
Wakati wanadhani wamefika eneo la sherehe ilidhihirika kwamba ni dhahiri walikuwa wamepotea njia.
Mara moja Mkewe akamshauri mumewe waombe msaada kwa watu wawaelekeze jengo sahihi na sehemu sahihi ya sherehe, maajabu mumewe alibakia kimya bila kuongea wala kujibu chochote.
Mzee John aliendelea kuendesha huku anatafuta jengo hadi alifanikiwa kufika na kupata jengo sahihi la sherehe.

Kihisia mkewe aliumia sana hasa kwa kitendo cha mumewe kubaki kimya na kuonesha kutomsikiliza na kumjali pale alipokuwa anamshauri watafute msaada kuulizia njia na jengo sahihi.

Kwa upande wa mke wake kitendo cha kutoa ushauri kwa mumewe ni kuonesha anampenda ndiyo maana alimshauri watafute msaada kwa watu wengine.
Na Mzee John kwa upande wake alikuwa amekwazika sana na kitendo cha mkewe kumshauri kwani mzee alihisi kama vile mke wake hamuamini na hatamfikisha kwenye sherehe. Kwake haukuwa ushauri bali Dharau na kuelezea kwamba mwanaume hawezi.

Tofauti kubwa iliyopo kati ya wanawake na wanaume ni kwamba wanaume huwa hawapendi kupewa ushauri au kushauri mtu hadi wao wenyewe waombe.
Pia wanaume wana asili ya kujitatulia Matatizo yao wenyewe isipokuwa aombe mwenyewe msaada.
Mkewe hakujua kwamba kitendo cha mumewe kupotea njia hakikumaanisha apewe ushauri bali atiwe moyo na support kwamba atapata njia na kuonesha kumpenda zaidi.

Ukweli ni kwamba mwanamke katika ndoa au mahusiano anapoamua kutoa ushauri ambao hajaombwa (unsolicited) au kujaribu kusaidia kiushauri mwanaume bila kuombwa huwa hajui ni kiasi gani huwa inachukiza sana mwanaume na matokeo yake unaweza kuona mwanaume anakujibu kwa mkato au mwanaume anakula jiwe na kukuacha umeumia hisia zako.

Unapomshauri mwanaume kwa jambo dogo kama kuendesha gari na kupotea njia mwanaume hujiona kama vile umemdharau kwa jambo dogo sana je jambo kubwa utamuamini?

Tangu kale wanaume ni mafundi, ni wataalamu, ni mashujaa, ni experts, ni watatuzi wa Matatizo sasa unapompa ushauri bila kuombwa ni kama unamfanya yeye hana lolote.

Naamini jambo la msingi ni wewe mwanamke kusoma saikolojia za mume wako na jinsi ambavyo huwa anaitikia ushauri wako, kwani kuna wakati unatakiwa kumtia moyo na kuonesha upendo kuliko kushauri au kulalamika tu kwamba hajaweza kufanya hiki na kile.

Pia kumbuka mwanaume kujiamini kwingi hutokana na mafanikio anayopata kutokana na ufanisi, uwezo na taaluma yake na kitendo cha kumshusha humuumiza sana.
Pia wanaume huwa hawapendi kuongelea kuhusu Matatizo yao hadi yeye mwenyewe akueleze na pia hupenda kutatua Matatizo kivyao kwani huamini kwamba likitokea tatizo lazima yeye ndiye atoe solution.

No comments:

Post a Comment