Tuesday, 14 July 2015

HASIRA KATIKA NDOA.

Linapokuja suala la hasira hakuna cha mweupe wala mweusi, hakuna cha mfupi wala mrefu, hakuna cha mnene wala mwembamba;
wote tunapata hasira na tunatofautiana katika kuithibiti hasira.Hasira ni hisia asili ambazo humtokea mtu yeyote.
Na hasira ni mwitikio wa mtu kutokana na hisia za usalama wake, furaha yake au amani yake na kila mmoja wetu amewahi kuwa na hasira na inawezekana hata sasa hivi unaposoma hapa bado una hasira ambazo zimekujaa kutokana na kuudhiwa bosi wako, mume wako, mke wako, mchumba wako, kiongozi wako, rais wako, watoto wako, wanafunzi wako au kitu chochote.

Watu tunatofautiana sana linapokuja suala la kiwango cha hasira na jinsi ya kuiyeyusha hiyo hasira.
Wapo watu akipata hasira hata kuongea hawezi kabisa na wengine wanakuwa wepesi hata kuzipiga, wengine akiwa na hasira anazira kabisa kufanya kitu chochote.
Migomo mingi mashuleni na makazini wengi huongozwa na hasira ndiyo maana wakati mwingine hufanya vitu vya ajabu.
Na wale waliopo kwenye ndoa naamini wanajua mengi sana kuhusiano na neno HASIRA kwani kupata hasira katika ndoa ni jambo ambalo halikwepeki kwani mnakutana watu wa malezi tofauti na aina tofauti ili kuwekana sawa lazima kuna vitu mmoja hatapenda na wakati mwingine kupata hasira.
Wengine akishakuwa na hasira kama ni kwenye ndoa basi ujue umeumia na ni kasheshe kwelikweli, maana kulala ni mzungu wa nne, chakula utajijua mwenyewe, inakuwa vita ambayo huna jinsi.
Wapo ambao pia akiwa na hasira ni kilio utadhani kuna msiba.
Kuna wengine ni mashujaa wa kukaa na hasira zaidi ya wiki, wengine zaidi ya mwezi na wengine zaidi ya mwaka pia wapo wengine hasira zao huishi kwa muda kidogo sana na hasira zikiisha anaweza kukuomba msamaha mara moja.
Na wengine akipata hasira atakununia tu hata kukusalimia hana mpango.

Hasira zinajenga au kubomoa na hili linatokana na mwitikio wako ukipata hasira.
Tatizo si kuwa na hasira bali ni jinsi gani una react ukiwa na hasira.
Watu wanaojifunza mambo ya hasira wamepata data zinazoonesha kwamba watu waliopo kwenye ndoa ndiyo wenye hasira mara kwa mara kuliko taasisi yoyote duniani.

Uthabiti wa ndoa unategemea sana ni jinsi gani wanandoa wana deal vipi wakiwa na hasira kwani ndoa nyingi zimekuwa hell kwa sababu ya wao kushindwa kuthibiti hasira zao.

IMANI POTOFU KUHUSU HASIRA
Kama kwa nje unaonekana huna hasira basi huna tatizo na hasira.
Ukijifanya huna hasira basi hasira huondoka yenyewe.
Kuwa mwema muda wote ni njia ya kuonesha kwamba hasira haiwezi kukuumiza
Ndoa yako itapata shida kama utaonesha kwamba umekasirika.

Wataalamu wa mambo ya hasira wanakiri kwamba hasira ni kitu kizuri kwenye mahusiano ya ndoa na ni kitu ambacho kipo katika ndoa zote na kwamba hasira huimarisha ndoa na huimarisha pale tu mnapotatua tatizo la hasira kwa njia ya kuelewana.
Kila mwanandoa ana haki ya kumruhusu mwenzake kuonesha hasira yake, kujieleza kwamba umekasirika na kueleza nini kimesababisha kupata hasira.
Kitu cha msingi ni wewe mwenye hasira kueleza kwa upendo, hekima na busara kwa mwenzako kwa nini umekasirika na nini kimesababisha upate hasira.
Unapopata hasira ni vizuri kuelezea hasira zako kwa maneno ya upole na kwa sauti ileile kama vile unapoongelea mambo mengine ukiwa na mpenzi wako.
Pia ni vizuri kwa mwanandoa kumsoma mwenzako mwitikio wake akiwa na hasira unatakiwa kufanya nini. Wapo ambao akiwa na hasira kaa mbali kwani baada ya muda hasira zake kuishi ndipo mnaweza kukaa na kujadili.

Kujua mwenzako amekasirika na kumruhusu kuelezea hasira zake tena kwa upole na moyo wa upendo ni vizuri kwani utakuwa mwanzo wa kujua tatizo lilikuwa ni nini hadi kupelekea yeye kukasirika na kujua tatizo ni kitu kizuri kwani utafanya juhudi kutorudia tena.

JINSI YA KUONDOA HASIRA
Kwanza ni kukubali kwamba una hasira yaani mwenzako ajue una hasira, ingawa ni rahisi sana kujua mke au mume wako sasa ana hasira.
Kwa kuwa una hasira usikubali kumaliza hasira zako kwa kuanza kumlaumu mwenzako.
Elezea kwa utulivu na upole kabisa kwa nini una hasira na kitu gani kimesababisaha upate hasira.
Jitahidi kuchukua hatua, fanya kitu ili kuondoa tatizo lililosababisha uwe na hasira.

No comments:

Post a Comment