Sunday, 28 June 2015

KUBEMENDA NI NINI?

Kubemenda ni imani potofu (myth) na hakuna uhusiano wa sperms na maziwa ya mama katika kudhoofisha afya ya mtoto; iwe kwa kushirikiana tendo la ndoa au kumshika mtoto baada ya sex.

Je, nini maana ya kubemenda mtoto?

Kwanza hii imani potofu inaeleza kwamba kubemenda mtoto ni pale wanandoa wanapojihusisha na tendo la ndoa baada ya mtoto Kuzaliwa (pale mke anapokuwa tayari kiafya kwa tendo la ndoa baada ya kujifungua) kwa maana kwamba sperms huharibu maziwa ambayo mtoto ananyonya, si kweli hakuna uhusiano wowote kati ya maziwa ya mama na sperms katika kuathiri afya ya mtoto.
Pili kubemenda mtoto ni kitendo cha wanandoa kujihusisha na tendo la ndoa na mke kushika mimba miezi mwili tu au mitatu tu baada ya kujifungua na kupelekea kuzaa mtoto mwingine baada ya mwaka na matokeo yake mtoto aliyetangulia Kuzaliwa huwa dhaifu kiafya (huchelewa kutembea) na huitwa ni mtoto ambaye amebemendwa, kitu ambacho ni imani potofu kwani kuna wanandoa wengi tu wamezaa watoto waliopishana mwaka na wote wana afya njema kabisa.
Tatu kubemenda ni kitendo cha mwanandoa mmoja kutoka nje ya ndoa (sex) na akirudi ndani huendelea na tendo la ndoa na matokeo yake mtoto wa ndani ya ndoa huwa dhaifu, pia ni imani potofu hakuna kitu kama hicho.

kuhusu tendo la ndoa jambo la msingi ni kufuata ushauri wa kitaalamu ambao ni wiki sita baada ya kujifungua.

Je, kuna ukweli wowote kuhusiana na hii imani potofu

Iwe wanandoa kujihusisha na tendo la ndoa baada ya mtoto Kuzaliwa au kuzaa mwingine baada ya mwaka au hata kutoka nje hakuna uhusiano na mtoto aliyezaliwa kama suala la usafi na lishe bora litazingatiwa kwa mtoto anayehusika.

Je, kulikoni mababu zetu wakaweka imani kama hiyo kwa wanandoa?

Kama zilivyo imani zingine potofu kama vile mwanamke mjamzito kutokula mayai mababu zetu walikuwa na somo ndani yake, inawezekana walitaka kuhakikisha wanandoa wanashiriki vizuri katika kulea mtoto kwa pamoja bila kupendekeza tabia za uchafu na kujirusha nje na ndani ya ndoa bila utaratibu.
Pia labda mababu zetu walihofia kitendo cha mwanamke kutoa maziwa (chuluzika) wakati wa tendo la ndoa hasa anapofika kileleni (tangu akifungue hadi miezi 8 hivi) na wakawa wanahofia kinaweza kuathiri kiwango cha chakula cha mtoto hivyo ili kuzuia ni kutunga imani (potofu) kwamba mtoto ataathirika kwa mke na mume kushiriki tendo la ndoa.

Je, ili mtoto asionekane amebemendwa wanandoa wanahitaji kufanya kitu gani?

Ni vizuri kufahamu kwamba hakuna uhusiano wa sperms kuharibu maziwa ya mama wakati wa kumnyonyesha mtoto hivyo wanandoa kushiriki tendo la ndoa halina uhusiano wowote na mtoto kuwa na afya mbaya kiasi cha kuchelewa kutembea.
Mtoto anahitaji chakula bora chenye viini-lishe vyote vinavyohitajika ili kukua vizuri pia mama anahitaji kujiweka mazingira safi (kuwa msafi) wakati ananyonyesha, ahakikishe anasafisha chuchu zake na mikono yake au kuzingatia usafi kimwili kabla ya kumnyonyesha mtoto iwe baada ya sex au muda wowote.
Ni jukumu la baba na mama wa mtoto kuhakikisha wanatumia muda wao kuhakikisha mtoto anapata lishe bora na mahitaji yote ya msingi ya mtoto ili kukua na kuwa na afya njema na si kujinyima kujihusisha na tendo la ndoa wakihofia mtoto kuonekana amebemendwa.
Pia suala la usafi wa mazingira ya mtoto anapoishi (vyombo vya kutumia kwa chakula cha mtoto, usafi wa mwili wa mtoto na mama na baba pia) ni muhimu sana kwani baada ya tendo la ndoa ni muhimu kwa mume na mke kuhakikisha wanakuwa safi tena bila kujihusisha na kumnyonyesha mtoto huku hawajanawa au kuoga.

No comments:

Post a Comment