Tabia ya kumpendelea mtoto mmoja au kila mzazi kuwa na mtoto wake ambaye anagusa zaidi moyo wake ipo sana katika familia zetu.Wengi huwa hawataki kulitaja au kuliongelea kwa undani ingawa ni kweli familia nyingi zitakiri kwamba hili ni tatizo sugu na pia inawezekana wewe ni mmoja ya watoto waliopendwa au ambao hawakupendwa na moja ya wazazi wenu.
1.Kwa nini upendeleo hutokea kwa mtoto mmoja?
Inawezekana tabia ya huyo mtoto ni njema zaidi kuliko wengine, wakipewa kazi mmoja anafanya na mwingine hafanyi mara zote, anayetii hujikuta anapendwa zaidi.
Inawezekana tabia ya huyo mtoto ni rahisi na mwenzake au wenzake ni ngumu.
Inawezekana mtoto anafanana na mzazi zaidi kuliko wengine (tabia na mwonekano).
Inawezekana huyo mtoto anafanikisha matarajio ya wazazi wake au mzazi mmoja.
Inawezekana kwa sababu ni mvulana peke yake au msichana peke yake mzazi hujikuta anampenda zaidi.
Pia inawezekana talents zake au vipaji vyake vinafanana na vile mzazi anataka mtoto awe au inawezekana ndiyo values za familia.
Pia inawezekana mtoto asiyependwa ni mtoto ambaye ni mbishi au ni mtoa hamasa (challenge authority) kuliko mwenzake au wenzake. Mtoto ana njia zake au mitazamo yake kuhusu maisha na vitu hivyo wazazi au mzazi hujikutana wanabishana kila kitu.
Pia kuna mazingira ya kuzaliwa ambayo hufanya mtoto kupendelewa zaidi ya wenzake kama vile mtoto kuzaliwa siku au wakati (huohuo) ambao mzazi wa baba au mama (babu au bibi) yake anafariki, ingawa haina ushahidi wa kisayansi ila matukio mengi huonesha kwamba mtoto wa aina hii huonekana wa thamani kuliko wengine na ni kama vile roho ya babu au bibi huenda kwa mtoto anayezaliwa na wazazi kujikuta wanampenda kuliko kawaida.
Au inaweza kuwa ngumu sana mzazi kuweka bond na huyo mtoto kutokana na huzuni, stress na depression mzazi alipata wakati anazaa na wakati huohuo mzazi wake mwenyewe (baba au mama) naye anafariki.
Mtoto kuzaliwa bila kutegemea hasa baada ya wazazi kudhani wamemaliza kuzaa.
Mtoto kuwa na matatizo ya afya hivyo wazazi kutumia muda mwingi kwake na wengine kujiona mwenzao anapendelewa.
Wakati mwingine inatokea tu mzazi hujikuta anampenda mtoto fulani katika familia kuliko wengine.
2. Nini mojawapo ya Dalili za mtoto kupendelewa?
Kununuliwa zawadi zaidi ya wenzake.
Kutoa adhabu rahisi kuliko wenzake kwa kosa moja, wenzake wanakula fimbo yeye anaonywa tu.
Sherehe au sikukuu zake kuwa tofauti na wenzake kwa jinsi zinavyoandaliwa nk.
Wenzake wakiomba kitu hichohicho wanakataliwa lakini yeye anapewa au kuruhusiwa.
Mzazi kutumia jina lake kumaanisha watoto wake wote kama vile baba anarudi kazini na watoto hawapo na mtoto anayempenda anaitwa Ben na badala ya kuuliza watoto wapo wapi yeye anauliza “akina Ben wako wapi?”
Tumia muda mwingi na mtoto mmoja.
Kuonesha upendo wa dhahiri kwa mtoto mmoja nk nk nk.
3.Je, mtoto ambaye anajisikia hapendelewi na mzazi au wazazi hujisikiaje?
Mtoto anakuwa na wakati mgumu sana kujikubali na kujipenda mwenyewe kwa kuwa anaamini mzazi/wazazi hawampendi na anaweza kuwa na tatizo sugu la kutojiamini (chronic low self-esteem)
Mtoto hujiona duniani hakuna haki na kwa kuwa hatendewi haki na yeye anaweza kuanza kutowatendea haki wengine.
4.Je, mtoto anayependwa anaweza kupata madhara yoyote?
Ukweli ni kwamba hata mtoto ambaye anajiona anapendwa pia anaweza kupata tatizo la kukosa kujiamini kwani anakuwa too much spoiled.
Kwa kuwa anapendwa basi atajitahidi kufanya zaidi kwani anaamini asipofanya kila kitu juu anaweza kupoteza kuendelea kupata upendeleo hivyo kama ni shule atajitahidi kupata grades za juu, kama ni tabia atajitahidi asikasirike nk na matokeo yake atakuwa hajiamini na anaweza kupota msongo mawazo.
Mtoto anayependelewa anaweza kuwa si mzuri sana linapokuja suala la wenzake wa rika moja au walimu au watu wengine kwenye maisha kwani kile kitendo cha kujiona anapendelewa na wazazi au mzazi humpa kakiburi Fulani.
Mtoto anayependwa hujiona yeye ndo mzuri na huwa hakosei hata hivyo maisha hayako hivyo na matokeo yake atakuwa na wakati mgumu mbele ya maisha hasa llikija suala la kupambana na matatizo.
Hasara ya kumpendelea mtoto mmoja huendelea hadi kwa wajukuu na inaweza kuleta matatizo na migogoro kwa kuwa wajukuu wa watoto wote huanza kuzozana kwa kuwa mmoja wa wazazi wao alikuwa anapendwa zaidi na babu au bibi.
5.Je, kwa mume na mke ni tatizo?
Ndiyo kunaweza kutokea mgogoro kati ya mke na mume hasa kwa mtoto mmoja kupendelewa na mzazi mmoja, kwa mfano baba anampa fedha nyingi zaidi mtoto mmoja anayempenda bila kujali ni mdogo kuliko wenzake, mama akiona au kusikia naye huja juuu kitendo ambacho kitafanya ndoa iwe katika mzozo.
6.Je, unaweza kuepuka vipi kumpendelea mtoto mmoja?
Kwanza wewe mzazi jikubali kwamba wewe ni binadamu na kwamba katika watoto wako mmoja anakubalika kwako zaidi kuliko wengine.
Wasikilize watoto wengine ambao wanakwambia unampendelea mwenzao na usijilinde, wasikilize na anza kufanyia kazi yale wanasema (kuacha kumpendelea mmoja)
Gundua utofauti wa kila mtoto na kile anapenda kufanya (characteristics, skills, interest) na mhudumie kutokana na vile anavipenda.
Usiwalinganishe au kumsema mmoja kwa sababu ya mwingine kwani kila mtoto yupo tofauti, sentensi kama “mwenzako Ben akirudi shule anafanya homework yake vizuri na anamaliza wewe hadi ulazimishwe!”
Ni kweli amekosea hata hivyo kila mtoto yupo tofauti na kila mtoto anatakiwa kuambiwa kama yeye na si mwingine.
Kama unanunua zawadi ni vizuri kununua zawadi zinazolingana siyo mmoja unanunua zawadi ya Tsh. 100,000 na mwingine Tsh. 20,000
Tumia muda vizuri na sawa kwa watoto wote.
Kumbuka jinsi unavyozidi kuwa na watoto wengi ndivyo utakuwa na kibarua kigumu zaidi, kwani unahitaji kutafuta muda maalumu kwa kila mtoto na kugundua kipaji chake na kuhakikisha unakiendeleza sawa na watoto wengine.
Jambo la msingi ni kila mzazi kumpa (treat) kila mtoto sawa katika hali zote na juhudi za ziada zinahitaji katika mazingira ya nyumbani kuhakikisha watoto wote wanalelewa sawa na kila mmoja kujiona ana thamani sawa kwa wazazi mmoja mmoja na kwa pamoja.