Katika maisha haya tunayoishi, wapo watu wenye tabia ya kutishia wenzao baada ya mizozo mbalimbali.
Yupo anayemtishia mwenzake eti asipoangalia atamuua, mwingine anamtishia kumnyima kitu fulani iwe fedha, chakula na kadhalika.
Kwa wengine matishio wanayotoa ni hasira tu wala hayamaanishi maamuzi ya kweli.
Kwa maneno ya mitaani huwa wanasema ``anamtishia nyau.
Huku wengine wakichukulia matishio mengine ni utani, hebu sikia kisanga hiki ambapo familia imejikuta ikisambaratika kisa mume kamtishia nyau mkewe kwamba atamuacha kama hakuwa makini.
Kisa hiki kanisimulia mama mwenyewe yaliyomkuta ambapo sasa anaishi na mume mwingine na tayari wamezaa mtoto mmoja.
Baba huyu (mume wa pili wa mama huyu), ni mume wa mtu mwenye familia yake inayoishi hapa hapa jijini.
Naam, ilikuwaje? Kwa mujibu wa simulizi ya mama huyu, aliwahi kuolewa na mwanaume mmoja wakazaa watoto wawili, msichana na mvulana. Mama akiwa anakaa nyumbani, huku mume akihangaika na biashara.
Mara kwa mara mume huyu akiwa anamwambia mkewe kuwa iko siku atamwacha.
Tishio hili, kwa mujibu wa mkewe lilikuwa linamkera sana. (hata hivyo binafsi siamini bwana yule alikuwa anasema vile bila sababu.
Lipo jambo ambalo mke huyu alinificha).
Naam. Baada ya mke kutafakari kwa muda, eti akaamua kutafuta chumba sehemu nyingine kwa siri bila mumewe kujua.
Baada ya kukipata, akatafuta mzozo ili apate mwanya wa kuondokea. Huku na huko akamvizia mume akiwa anakula na kumuuliza; hivi hilo tishio kwamba iko siku utaniacha lina maana gani? Mume akahamaki na kusema; unadhani utani? Nitakuacha kweli, wanawake mbona tele, hujui mke mmoja anakinaisha? Maneno hayo kwa mujibu wa mama huyu yalimchefua kweli kweli. Lilizuka zogo la kishoka ambapo (mama aliamua kwenda kulala. Asubuhi mume akaenda kazini kwake hadi jioni.
Huku nyuma mama akafungasha vitu vyake akavipeleka kwenye makao yake mapya, kisha kurejea ili amsubiri mume amuage. Ilikuwa ni kichekesho kitupu.
Bwana kurejea nyumbani alimkuta mke akiwa sebuleni huku kashika tama (mkono shavuni). Mume kuuliza kulikoni ``nilimjibu nimesubiri nikuage, si umekuwa ukiniambia iko siku utaniacha? Sasa hivi naondoka, siwezi kuvumilia kuachwa heri nikuache wewe mapema, watoto wako nakuachia pia japo huyu wa pili ni mdogo, kwa heri ya kuonana? Mpenzi msomaji, hivi ndivyo mama huyu alivyoondoka kwa mumewe kama alivyonisimulia mwenyewe.
Bwana yule hakuamini macho wala masikio yake akabakia ameduwaa asijue la kusema.
Pengine alikuwa akijutia kauli yake ya kumwacha mkewe siku moja. Kwa mujibu wa mama huyu kule makao mapya akatafuta sehemu ya kupikia vyakula (mamantilie) akafanikiwa na ndipo akampata mzee mmoja aliyekuwa mteja wake na katika mazungumzo ya mara kwa mara wakawa wapenzi na sasa mzee huyu amempangishia chumba eneo jirani na anakofanya kazi. Na siku mama huyu ananisimulia kisa hiki walikuwa wote na mzee pamoja na mtoto wao.nilipotaka kujua mume wa awali wa mama huyu yuko wapi niliambiwa tayari alishafariki. Pia mmoja wa watoto (yule mdogo) naye aliugua akafariki ambapo yule mkubwa ameolewa na ameshazaa.
Mwanamama huyu anasema amejaribu kumsaka bintiye huyo bila mafanikio. Yasemekana baba yake kabla ya kuaga dunia aliagiza kuwa mtoto huyo asipewe mamake kutokana na ukatili aliomfanyia wa kumuacha huku bado alikuwa anampenda kwa dhati. Hakika, Maisha Ndivyo yalivyo.
Jamaa alifikiri anatishia nyau kumbe yakawa ni kweli. Kisa hiki kinatukumbusha kuwa makini na kauli tunazotoa midomoni mwetu kwani zingine ni mauti kwetu.
Hata hivyo yawezekana mama na baba wa familia niliyogusia hapo juu, wote walikuwa na matatizo Fulani ambayo hayakuwa dhahiri.
Mume kumtishia kumwacha lazima lipo jambo alilokuwa akifanya mkewe lisilompendeza.
Na mke huyu pengine naye alishamchoka mumewe hivyo kutafuta sababu za kutengana au kuachana.
Huwezi kujua. Nyumba za watu zimeficha mengi.
Utaona baba na mama wakicheka pale wanapokuwa na wageni sebuleni, lakini wakiondoka huo moto unaowaka humo ndani ni balaa tupu. Wengine hawalali chumba kimoja au kitanda kimoja. Wengine tokea wanaingia garini kwenda kazini hadi wanafika hawaongei, hawacheki.
Maisha gani hayo?
Tumrudie Mungu abariki nyumba zetu.
Kwani amri kuu aliyotuachia `upendo tupendane`, tumeiweka kando. Turejeshe upendo ili amani na utulivu vitawale maisha yetu.
Niwatakie Jumapili njema.
No comments:
Post a Comment