Saturday, 24 January 2015

SIMU ZINAVYOHARIBU MAHUSIANO

Mwanaume hata mwanamke ukiona simu yake ina password au anaichunga sana hata akiwa nyumbani, ujue hapo hakuna uaminifu.
Kama nilivyoizungumzia simu wiki jana kuwa makusudia ya mtu aliyeitengeneza kusudio lake kubwa lilikuwa kurahisisha mawasiliano si kingine. Lakini wanadamu wenye mioyo dhaifu tumeitumia kama kichaka cha kuficha maovu yetu.
Sasa hivi ndani ya nyumba simu imekuwa chanzo cha kuvunjika kwa amani, asiye muaminifu uilinda simu yake kama ikulu ya Barack Obama.
Sasa hivi ndani ya nyumba zetu inaonyesha jinsi gani zimepoteza uaminifu kila mmoja analinda simu yake kuliko hata wivu kwa mwenzake.
Imekuwa kila mmoja anamwinda mwenzake alale ili aipekue simu, kwa vile ni mzoefu hata ukibahatika kuipata utakuta uchafu wake amefuta ili kupoteza ushahidi.
Ukiona hivyo mnakuwa mnaishi kwa mazoea lakini fahamu hakuna upendo ndani ya nyumba yenu na kuvunja ile ahadi ya kuishi kwa upendo na uaminifu katika ndoa.
Unaweka password unamuonyesha nini mwenzako? kama mwanaume unamuonyesha kabisa mkeo kwamba una wengine zaidi yake hapo unamfundisha nini mkeo, akilipa kisasi umlaumu nani?
Nimekuwa nikisema kila siku kuhusu uaminifu ili tuangalie unachokifanya ni sahihi na ndiyo mapenzi?
Nilielezea mapenzi ni kupendana kuheshimiana kuoneana huruma kujaliana na uvumilivu.
Nilielezea mapenzi ni kupendana, kuheshimiana, kuoneana huruma, kujaliana na kuvumiliana. Ukiwa na mapenzi lazima utakuwa na vitu hivi kwa mwenzako, pia utakuwa muwazi kwake na mkweli ili kufanya muweze kuishi bila mmoja kuwa na mashaka na mwenzake.
Wapendanao siku zote hulinda heshima yao kwa kila mmoja kuilinda ya mwenzake, pia kuwa wawazi ili chochote kitakachokwenda kinyume, kiulizwe na kupatiwa majibu sahihi bila kujiumauma. Pia huwa hawana mipaka kuanzia katika miili yao na vitu vyote kwa vile huamini wao ni kitu kimoja, hivyo hawafichani kitu.
Watu kama hawa simu si chanzo cha matatizo, bali ni chombo cha mawasiliano, hakuna mtu wa kuificha simu yake wala kuweka password na kila mmoja ana uhuru wa kuishika au kuopokea ya mwenzake.
Nina imani somo langu limesomeka vizuri, sasa tunarudi kwenye mada ya leo kwa kuuliza swali, sifa nilizozieleza kuhusu mapenzi, je, wewe unazo au mwenzako anazo? Je, simu katika nyumba yenu inatumikaje? Ni chanzo cha migogoro au ni chombo cha mawasiliano ambacho kinaachwa popote bila masharti yoyote?
Tutumie simu kama chombo cha mawasiliano, hata kama si muaminifu katika uhusiano, si lazima mwenzako ajue jinsi gani unavyomdharau kupitia simu.
Simu isiwe chanzo cha migogoro na kuvunja nyumba zetu ambazo sasa hivi zimeingia mdudu ambaye ameonyesha jinsi gani tusivyo waaminifu, kitu ambacho kimeongeza ukosefu wa amani katika ndoa zetu.
Tuwe wawazi na wakweli kwa wenzetu, tuone aibu kuonyesha kwa vitendo sisi si waaminifu. Kama ulijua wazuri kuliko mwenzako wapo wengi, ulikaa naye kwa sababu gani?

No comments:

Post a Comment