Friday, 16 October 2015

BADO UNATESWA NA MAPENZI?

Yawezekana hadi sasa bado kuna mtu anakusumbua, umejaribu kumbembeleza lakini hataki kukubaliana na wewe, huyo hakufai.

Mapenzi hayapo ili yatutese,  badala yake mapenzi yapo kwa ajili ya kutupa faraja maishani mwetu.

Muondoe kabisa akilini mwako mtu wa aina hiyo, kwani atakufanya uyaone maisha kwa mtazamo hasi jambo ambalo siyo zuri.

TUFANYEJE ILI MAPENZI YASITUTESE?
Hili ni swali ambalo kwa hakika linahitaji majibu yakinifu, ili kuondoa vilio vya mapenzi vinavyowakumba watu wengi kila kukicha, kama nilivyoeleza huko nyuma kuwa, mapenzi yana kanuni zake ambazo zinatakiwa kufuatwa ili kuepusha upande wa pili wa shilingi ya  mapenzi, upande wa maumivu.
 
UAMINIFU
Hii ni suala la kwanza kabisa katika kuepuka maumivu ya mapenzi, kwani ukiwa mwaminifu katika ndoa au uhusiano wa kimapenzi ulionao, basi itakuwa ni vigumu kwako kuteswa na mapenzi maana utakuwa umefuata moja ya kanuni zake.

Si jambo la busara kuwa na wapenzi zaidi ya mmoja ukidhani ni ujanja au ni kwenda na wakati, la hasha, mapenzi hayaendi hivyo na usipokuwa makini utaishia kulia kila mara.

Utakapobainika kuwa wewe si mwaminifu, watu wengi watakutumia kimapenzi kwa faida zao na mwisho watakuacha ungali bado unawahitaji na hapo ndipo mwanzo wa chungu ya mapenzi huanza, yaani kuachwa na mtu ambaye bado unampenda.

Kwa waliowahi kutokewa na hali hiyo, wanaelewa namaanisha nini. Acha kurundika wapenzi. Jiheshimu na  mapenzi yatakuheshimu.

UONGO
Sumu yenye nikotini kali katika mapenzi ni uongo, kama wewe ni mzuri wa kupiga porojo katika uhusiano wako, basi mapenzi ni lazima yakutese.
 
Kwa nini uwe muongo katika mapenzi? Kuna faida gani ya kuwa na wapenzi wengi? Kwanini mapenzi yanakuumiza?

Leo uko na huyu, kesho uko na yule, maisha hayo hadi lini rafiki yangu? Utaishia kuwadanganya wanawake hadi lini ndugu yangu na wewe mwanamke, utawapanga hao wanaume hadi lini? Unadhani kuwachuna hao mabwana ndiyo maisha yanaishia hapo?

Tuachane na maisha ya kutangatanga na mapenzi, badala yake tuhangaikie maisha yetu.

Je, bado mapenzi yanakutesa? Umechelewa, kwani muda unaoupoteza katika kuhangaikia mapenzi, unatakiwa kuutumia kuwaza mambo ya muhimu ili mwisho upate maendeleo.

Kama una mpenzi au bado hujampata, basi vuta subira atakuja. Jambo moja la muhimu kuamini ni kuwa kila mmoja ana mwenza wake maishani, tatizo linakuja pale tunapoishiwa na uvumilivu na badala yake tunageuka watu wa kudandia na kubadilisha wapenzi kama nguo kila kukicha.

Kusema ukweli hayo siyo  maisha. Vuta subira, msubiri wako yuko njiani anakuja, na kama umeshampata, basi tulia naye huku mkipanga mikakati ya mafanikio kwenye ulimwengu huu uliojaa ushindani.
Hivi sasa maisha ni magumu, inakuwaje unakubali mapenzi yakutese?

Siwazuii watu kupenda, lakini  waache kuyapaparukia mapenzi kwa kutofuata kanuni zake. Yataishia kutuliza kila kukicha.

Mapenzi yapo tangu enzi za mababu zetu, kwa nini kuyaendea pupa, epuka sana kunga’ng’ania mapenzi kwa mtu asiye na chembe hata moja ya mapenzi juu yako, kwani kufanya hivyo ni kuzidi kujiletea mateso  maishani.

Napenda kuhitimisha kwa kusema kuwa, wewe ni mzuri mno, mapenzi yasikuumize kwani wako wa maisha yupo lakini bado hamjaonana na mkikutana haitakuwa shida kuanzisha uhusiano kwani mapenzi ya dhati huwa kama sumaku na chuma ni lazima vivutane.

Mwisho kabisa, waza sana juu ya maendeleo ya kimaisha na si mapenzi, kama unafanya kazi basi ongeza ufanisi kazini ili baadaye uishi maisha bora wewe na mkeo au mumeo kwa kuwa na mahitaji muhimu katika familia.

No comments:

Post a Comment