Wednesday, 8 April 2015

JE,UNAMPENDA AU UNAJILAZIMISHA?...Jipime kwa maswali haya

Watu wengi wako kwenye uhusiano wa kimapenzi bila kujua kama kweli wanapenda kwa dhati au wanajilazisha? Ili kutambua upendo wako jipime kwa maswali yafuatayo:

1 - Unapoamka asubuhi wazo la kwanza kukujia linamhusu mpenzi wako au unafikiria zaidi kazi na mambo mengine? Una msukumo wa kutaka kumsalimia na pengine kumuuliza anapenda afungue kinywa kwa chakula gani?

2 - Je umekuwa mwepesi na mwenye furaha kubwa kuwaambia rafiki zako wa karibu juu ya hisia zako kwa mpenzi wako? Unajisikiaje wanapokushawishi vibaya kuhusu yeye?

3 - Je, anapokwambia anakuja kukutembelea huwa unajisikia hamasa moyoni kiasi cha mwili kusisimka?

4 - Unapokuwa peke yako mawazo yako yanatawaliwa na yeye au unafikiria kucheza gemu kwenye simu yako na kujifariji kwa vitu vingine?

5 - Unapompima kwa kumlinganisha na wengine anachukua nafasi ya kwanza au anazidiwa?

6 - Je, unapomfikiria na kupata kivutio fulani ndani ya moyo wako kuhusu ucheshi na utani wake huwa unatabasamu hata ukiwa peke yako?

7- Unajisikiaje wazo la kusalitiwa linapokujia, unaona ni sawa au unahuzunika kiasi cha kupoteza furaha na kutamani uambatane naye kila aendako ili usiibiwe?

8 - Hebu jiulize ni mara ngapi umekuwa ukishawishika kumnunulia mpenzi wako nguo, mapambo au vitu kwa lengo la kumfanya avutie au ndiyo umemtelekeza na kumwacha aonekane mchafu na asiyevutia mbele za watu?

9 - Je, umekuwa mtu wa kujijali mwenyewe kwa mavazi na mwonekano wako kwa lengo la kumfanya mwenza wako afurahie kuwa na wewe au ndiyo unajiweka katika mazingira ya ovyo yanayomtia aibu kwenye jamii?

10 - Unapoota ndoto za kimapenzi usiku, amekuwa akikutokea yeye au kuna wanaume/wanawake wa pembeni ndiyo wanajitokeza katika kuota kwako?

11- Unaposikiliza nyimbo za kimapenzi huwa unahisi ujumbe huo ni kwa huyo umpendaye au unauelekeza kwa mtu mwingine?

12 - Je, marafiki wa karibu wa mpenzi wako wamekuwa wakikupa kipaumbele au wanakudharau na kutopenda kukutana na wewe?

13 - Unajisikia furaha kuwa naye au huwa unapenda ubaki mwenyewe nyumbani ili ufanye mambo yako unayodhani uwepo wa mpenzi wako ni kikwazo?
14 - Je, umekuwa ukitafuta kwa nguvu nafasi za kukutana na mwezako au ndiyo kila siku uko bize na kazi?’

15 - Unapomtathmini mpenzi wako unajiona umepata au umejishikiza wakati ukitafuta mwingine?

16 - Umekuwa mwepesi kiasi gani kukumbuka ahadi zako kwake au kila unachopanga kumfanyia unasahau? Kumbuka kuhusu kumpigia simu, umekuwa ukijikuta ukisahau mara kwa mara?

17 - Vipi mpenzi wako anapopata nafasi ya kukushika sehemu yoyote mwilini wako, huwa unahisi msisimko mkali au mpaka ulazimishe hisia?

18 - Je, uko tayari kumwamini kiasi cha kumwekea dhamana?

19 - Kama utasikia mpenzi wako anakusifia kwa wenzake au kukuthamini kwa lolote utajiona mwenye bahati duniani?

20 - Unapofikiri hadhi yako unaona inalingana na mwenzako au unahisi umemzidi na kwamba mapenzi yako ni kama umemsaidia kumweka juu?

21 - Unapopata siku ya kupumzika, mtu wa kwanza kumpa kipaumbele cha kujumuika naye ni huyo mpenzi wako au unapenda kufanya mambo mengine?

22 - Je, umekuwa ukitamani kumpigia simu kwa lengo la kusikia tu hata sauti yake na ukahisi furaha?
Mpenzi msomaji wangu, haya ni baadhi ya maswali ya msingi ambayo majibu yake yanaweza kukusaidia kujua kama unampenda au unaulazimisha moyo wako. Naomba ukae peke yako na ujibu maswali haya ambayo mengi yako kwenye msingi wa jibu la ndiyo au hapana.

No comments:

Post a Comment