Friday, 12 December 2014

SABABU ZA WAPENZI KUCHOKANA.

UNAWEZA KUDHIBITI KUCHOKANA?
Ndiyo! Inawezekana kabisa. Ni kweli wapo wengi ambao hujikuta tu wamewachoka wapenzi wao. Pengine hawataki hali hiyo na wanajitahidi kushindana nayo sana, lakini wanashindwa.
Si kwa kutaka ni kwa vile hawajui kitu cha kufanya. Hapa kwenye All About Love nitakusaidia cha kufanya. Twende sasa...
KUOGA PAMOJA
Wanandoa kuoga pamoja ni tendo linaloleta msisimko wa aina yake. Mara nyingi, ndoa inapokuwa changa kabisa, wengi huwa na mazoea haya, lakini wakishazoeana na ratiba kubadilika hili husahaulika.
Utakuta baba anarudi usiku sana, ameutwika vya kutosha, mke amejichokea, kaamua kuoga mwenyewe na baadaye amekula. Anamsubiri mume. Akifika anaingia bafuni peke yake, anarudi chumbani wanalala, asubuhi mchaka mchaka wa kwenda kazini, zoezi hilo haliwezi kufanyika tena.
Ikumbukwe kwamba, kwa kuoga pamoja huzidisha msisimko wa mapenzi na si ajabu hisia za mapenzi zikaamka kwa kasi ya ajabu na baadaye mambo yakaendelea vizuri chumbani. Kwa kuacha kuoga pamoja hupunguza msisimko na ndiyo mwanzo wa kuzoeana na kuchokana.
Ni vigumu sana kuanzisha suala la mapenzi chumbani kwa ghafla tu...huanzia mbali, ikiwemo wakati wa kuoga pamoja. Bila shaka nimeeleweka marafiki zangu. Angalia kipengele kinachofuata...
KULA PAMOJA
Silaha kubwa ya kutochokana ni kufanya mambo mengi kwa pamoja. Inaeleweka kwamba, majukumu ya kila siku husababisha watu kuwa mbalimbali kwa muda mrefu hasa nyakati za mchana, lakini angalau mkipata muda wa kula pamoja, mtakuwa karibu.
Mtasogezana karibu kihisia. Hata kama mnafanya kazi ofisi tofauti, mnaweza kupanga ratiba angalau mara moja kwa wiki, mkatoka mchana na kupata chakula pamoja. Muhimu zaidi ni usiku, wakati wa chakula cha jioni ni vyema wanandoa wakapata muda wa kula pamoja.
Kukaa meza moja huongeza msisimko, utani kidogo tu mtakaofanyiana au kulishana, unaweza kujenga kitu kikubwa na kila mmoja akabaki akimuona mwenzake mpya kila siku.
BUSU
Mwaaa! Tendo dogo sana lakini lenye msisimko wa kipekee. Jenga mazingira ya kumbusu mpenzi wako kila mara. Usikubali kumuacha hivi hivi, hasa kabla ya kulala, kuamka na kuagana naye.
Mbusu shavuni, halafu mwambie: “Nakupenda sana.” Wengi (hasa wanawake) husisimka sana wanapobusiwa shavuni au shingoni. Jizoeshe mtindo huu na kamwe hutajikuta ukimchoka mpenzi wako.
Busu ni alama kubwa ambayo unaweza kumuacha nayo akiikumbuka siku nzima. Atakuchokaje?
KUKUMBATIANA
Tendo hili huambatana na busu. Unaweza kuona ni mambo ya Kizungu sana, lakini hata mnapokuwa peke yenu sehemu ambayo hamuonekani unaweza kumkumbatia mwenzako na kumuongezea msisimko wa kuwa na wewe.
Siku za mwanzo za ndoa, wengi hulala wakiwa wamekumbatiana lakini baadaye tabia hii hupotea ghafla. Hili ni tatizo. Mkumbatie mpenzi wako usiku. Wanawake wengi hulala usingizi mzuri zaidi wanapolala juu ya vifua vya wanaume zao. Kwanini usiwe wewe?
Msogeze karibu yako, mbembeleze ajilaze juu ya kifua chako akideka. Kiukweli utafurahia mapenzi na utajikuta unaendelea kumpa mpenzi wako nafasi ya kwanza kila siku.

No comments:

Post a Comment