Tuesday, 16 December 2014

UTENDEE HAKI MOYO WAKO.

HEBU jiulize kwa nafasi yako hapo ulipo, unautendea haki moyo wako? Mpenzi uliyenaye unampenda au unajilazimisha kuwa naye?

Elewa kuwa mapenzi ni sehemu ya maisha yetu na kwa hakika maisha yetu hayawezi kukamilika bila kuwepo mapenzi.Ninapozungumza juu ya mapenzi namaanisha yale yanayotoka moyoni mwa mtu mmoja kwenda kwa mwingine.

Mapenzi ya dhati ambayo hayachagui fedha wala dhiki, ambayo hayatofautishi sherehe na huzuni, maradhi na faraja!. Moyo wako ukubali kwa dhati na kwa hali zote kama nilivyoeleza hapo juu.

Mapenzi hukamilika baada ya wawili kuwa na hisia sawa za mapenzi. Amini kama upo katika uhusiano na mpenzi ambaye hakupendi, yaani wewe peke yako ndiyo unayempenda, wewe ni mtumwa wa mapenzi! Kama ndivyo, kwa nini uwe mtumwa?

Unadhani hakuna mwingine ambaye anaweza kukupenda kwa mapenzi ya dhati na penzi hilo likawa kwa pande zote mbili tofauti na ilivyo sasa?

Inawezekana huna sababu ya kulazimisha penzi kwa mtu ambaye hakupendi! Mapenzi ni nguzo ya maisha yetu, kama ukifanikiwa kumpata mpenzi ambaye atakupenda na wewe ukampenda ni wazi kuwa maisha yako yatakuwa yenye furaha na hakika utafurahia sana maisha yako na huyo mwandani wako!

Mapenzi yapo hivyo na kama ukijaribu kuyabadilisha utaumia mwenyewe! Wakati mwingine unaweza ukapendwa na mpenzi ambaye hujampenda, unadhani kuna ulazima wa wewe kulazimisha kumpenda?

Moyo wako umeshazungumza na wewe, umekuweka wazi kuwa hauna mapenzi ya dhati kwa mtu huyo, kwa nini ujilazimishe? Tatizo hili mara nyingi huwa kwa wanawake zaidi!

Anatokea mwanaume anampenda sana, anapomtongoza anajikuta kuwa hampendi, anachokifanya ni kumwambia kuwa atamjibu baadaye! Lengo la kumwambia hivyo ni kwa ajili ya kujipanga na kufikiria. Hakuna mapenzi ya aina hiyo, Hisia hazifikiriwi! Kama mtu unampenda, unapomuona tu siku ya kwanza, moyo wako hutetemeka juu yake na hutamani uambiwe kitu fulani na huyo aliyeuteka moyo wako ghafla.

Hii ina maana kuwa atakapokuambia kuwa anakupenda, huwezi kusubiri zaidi, hutakuwa na kitu cha kusubiri, ni nafasi uliyokuwa ukiisubiria kwa hamu kubwa sana.

Hapo sasa lazima utamkaribisha! Huo ndiyo ukweli. Moyo wako unapaswa kuwa muamuzi wa mwisho na siyo kuingia kwenye uhusiano ukiwa huna mapenzi kwa nia ya kujifunza kupenda.


Posted via Blogaway

Sunday, 14 December 2014

MAMBO YENYE THAMANI KATIKA MAPENZI.

Kila siku tunapaswa kujifunza zaidi kuhusu uhusiano na mapenzi maana maisha yetu hatuwezi kuwakwepa wenzi wetu hivyo ni vyema kujua mbinu mpya kila wakati za kuwafanya wenzetu wafurahie uwepo wetu.

Nimekuwa nikisisitiza mara kwa mara, usimwonyeshe mpenzi wako kuwa hana thamani. Mpe nafasi akueleze hisia zake. Kumsikiliza na kujua kilicho moyoni mwake kutakurahisishia kuishi naye kwa furaha maana utakuwa unafanya mambo ambayo yanampendeza.

Kuna mambo mengi ambayo ni muhimu sana kwa wapenzi. Unajua kuna vitu ambavyo wengine wanaweza kuvidharau na kuviona vya kawaida lakini kumbe vina thamani kubwa sana.

Mfano wanawake wengi huwa bize kuhakikisha wanaume wao wanakuwa wenye furaha na wanajiona wapo peke yao kwenye uhusiano. Ni jambo zuri, lakini kwa wanaume ni tofauti kabisa.
Hawana muda wa kuangalia mambo ambayo yanaweza kuwa kivutio kwa wenzi wao. Hilo ni tatizo kubwa sana kwenye uhusiano. Kwa bahati nzuri ni kwamba, wanawake huwa wanafurahishwa na mambo madogo sana.

Wanapagawishwa na vitu vya kawaida sana ambavyo vipo ndani ya uwezo wa mwanaume. Hebu twende tukaone vitu vingine ambavyo huwachanganya wanawake.

UJUMBE WA MAHABA

Kumtumia mpenzi wako au mkeo ujumbe wa mahaba ni sehemu ya kumwongezea ‘uchizi’ katika penzi lenu. Wengi hawapendi na pengine hawawezi kutunga meseji za kimahaba.
Kwa bahati nzuri ni kwamba, siku hizi za utandawazi mambo ni rahisi sana, magazeti mengi yanaandika Love Messages – za Kiingereza na Kiswahili.

Achana na magazeti hata baadhi ya kampuni za simu hufanya hivyo. Kwa gharama ndogo unaweza kujiunga na huduma hiyo kisha ukawa unatumiwa meseji kila siku.

Mitandao mbalimbali ya kwenye kompyuta nayo huandika meseji mbalimbali. Kitu cha kufanya hapo ni kukopi kisha kurekebisha kidogo kama utaona kuna vitu vya kuboresha kidogo, kisha mtumie mpenzi wako.

Unaweza kuona ni kitu kidogo sana, lakini utaona atakavyozidi kukupaisha kithamani katika maisha yake. Kama ulikuwa hujawahi kufanya, hebu anza utaona faida yake.
Fanya hivyo kulingana na nyakati, mfano asubuhi njema, mlo mwema, usiku mwema nk. Ni utaratibu mzuri sana kimapenzi.

MITANDAO YA KIJAMII
Siku hizi kuna mitandao mingi ya kijamii. Kwa bahati mbaya, baadhi ya watu huitumia vibaya na kuanzisha uhusiano usiofaa huko. Wanawake wengi huwa hawana amani na wanaume zao hata kama kwenye maelezo yao ya utambulisho wameandika wameoa au wana wachumba.

Kuweka picha yake mara chache au maneno ya kuonyesha unavyompenda, huziba hisia zake mbaya na kujiona yuko na mwanaume huru na makini.

Lakini hata hivyo, utakuwa umejiwekea ulinzi madhubuti na kuwafanya wanaofikiria kuwa na wewe wabadili mawazo yao wakijua kuwa nafasi imejaa! Jaribu utaona ukweli wa ninachokisema.

KUWA HURU NAYE
Wanaume wengi hawapendi mahaba, lakini asikudanganye mtu, kuongozana na mwenzi wako huongeza msisimko na kumfanya azidi kuwa huru na mwenye kujiamini. Usimwogope, mshike mkono, tembeeni huku mnamzungumza.

Kichwani hujiona mwanamke kamili, aliye na mwanaume asiye na ‘vimeo’ mitaani. Haya ni machache kati ya mengi ambayo kwa hakika hustawisha penzi.


Posted via Blogaway

Saturday, 13 December 2014

JE,UNATAKA KUPATA MKE/MUME WA KWELI ?

Kwanza wewe kama mwanamke/mwanaume mwenyewe unatakiwa ujifahamu na kufahamu vigezo vya mpenzi unayemhitaji katika maisha yako.
Wanawake/wanaume wengi hawajui wanahitaji wapenzi wa aina gani, hivyo wanajikuta kama watu wanaoingia sokoni bila kujua wanataka kununua nini? Ndiyo maana wengi wameangukia kwa matapeli wa mapenzi, wakachezewa na kuumizwa moyo bure.

SIFA ZA UMTAKAYE
Keti chini na kuorodhesha vigezo vya mwanaume/mwanamke unayemtaka. Baada ya hapo orodhesha tena kasoro za mwanaume/mwanamke unazoweza kuzivumilia na zile ambazo huwezi kuzivumilia kabisa. Hii inatokana na ukweli kwamba mwanadamu hajakamilika, ana upungufu wake.  

TUMIA MACHO
Anza kumsaka huyo mwanaume kwa kutumia milango ya fahamu. Cha kufanya hapa ni kuruhusu macho yawaone wanaume/wanawake na kuwatathmini kwa maumbile yao ya nje na kisha kupata majibu kutoka moyoni juu ya kuvutia kwao ambako hutambulika kwa moyo kuridhika na mwili kusisimka.

JENGA MAZOEA NAYE
Kuanzisha safari ya kuchunguza tabia za nje na za ndani kivitendo. Hapa suala la ukaribu baina ya mwanaume na mwanamke linahitajika. Msingi unaotajwa hapa ni kujenga mazoea ya kawaida yasiyokuwa na masuala ya kimapenzi na ngono. Kutambuana, dini, viwango vya elimu, kabila na makundi ya marafiki ni mambo ya kuzingatia.

Katika uchunguzi huu mwanamke/mwanaume anayetafuta mpenzi hana budi kupitia na kumlinganisha huyo aliyempata na vigezo alivyojiwekea. Zoezi hili liendane na kuweka alama ya pata kila anapobaini kuwa mwanaume/mwanamke anayemchunguza amepata moja ya vigezo vyake. Lakini pia aweke alama ya kosa kwa kila kasoro anayoivumilia na ile asiyoivumilia.

HAKIKI SIFA ZAKE
Jipe muda wa kutosha kati ya miezi sita na mwaka kumchunguza huyo mwanaume, kisha keti chini na anza kujumlisha alama za vigezo ulivyovijiwekea na jinsi mwanaume huyo alivyopata au kukosa.

Ikibainika uliyechagua amepata zaidi ya nusu ya alama ya vigezo vilivyowekwa, basi ujue kuwa anafaa. Kuhusu alama chache alizokosa unaweza kumsaidia kuzikamilisha pole pole mkiwa kwenye maisha ya ndoa.

Lakini angalizo kubwa kabisa ni kwamba mwanaume/mwanamke akionekana kuanguka katika kasoro zisizoweza kuvumilia kwa zaidi ya alama tatu. Yaani kwa mfano ni mlevi, mwizi, muongo, mbishi na katika hizo kashindwa 3, huyu hafai, ni vema akawekwa kando kwani huwezi kubeba kero 3 kwa pamoja katika maisha.

WEKA MALENGO
Lazima baada ya kuchunguzana kwa kina wapenzi watengeneze muongozo wa mapenzi yao. Wasiwe kama wanyama, lazima mipango ya wapi wametoka walipo na wanapokwenda waifahamu.
Hata hivyo, wataalamu wanasema lazima wapenzi wapime umakini wao kwa vitendo. Kama wamekubaliana kuoana, suala la mume kwenda kujitambulisha kwa wakwe na hatua ya kuiendea ndoa ionekane. Usiri usiwepo tena. Kila mmoja amuone mwenzake kama sehemu ya maisha yake na mara zote wasaidiane kwa ukaribu.

USHIRIKI WA NDUGU/MARAFIKI
Ni vema ndugu wakashirikishwa ili kuwapa nafasi na wao ya kuamua kama mapenzi hayo ni budi yakaendelea au yakasitishwa. Ni ukweli ulio wazi kwamba licha ya wengi kupuuza maamuzi ya ndugu kwa madai ya kuwa hawana nafasi kwa wapenda nao, lakini uchunguzi unaonesha kuwa wapenzi wengi huachana kutokana na sumu za ndugu hasa pale wanapokuwa wameonesha kutounga mkono uhusiano wa wanaotaka kuoana.

TENDO LA NDOA
Hatua hii ni ya kuweza kuzungumzia ufanyaji mapenzi, hapa nina maana kama wapenzi wamejizuia kwa muda mrefu na wanahisi kuchoka wanaweza kujadiliana kuhusu tendo la ndoa na kuamua kuwa pamoja huku wakizingatia suala la afya na uzazi salama.

NDOA
Kutimizwa kwa ahadi ya kuoana ni hatua ya tisa ambayo nayo si vema ikachukua muda mwingi kutekelezeka, kwani ucheleweshaji mwingi wa ndoa nao huvunja moyo na mara nyingine umewafanya wengi kutoaminiana.

UVUMILIVU
Kuamua kuwa mwili mmoja kwa kuvumilia na kuwa tayari kukabiliana na changamoto zote za maisha ukiwemo mkwamo na dhiki ambazo huchangia sana ndoa nyingi kuvunjika. Hapa pia ni wajibu wa wanandoa kuchukuliana udhaifu na kusaidiana.

Kuwa tayari kujifunza na kujali zaidi upendo kuliko hisia za mwili ambazo wakati mwingine hudanganya hivyo kumfanya mwanandoa asivutiwe na mwenzake.

Friday, 12 December 2014

FAIDA ZA KUMSIFIA MPENZI WAKO.

Kuna mengi mazuri ambayo huenda mpenzi wako aliwahi kukufanyia, je uliwahi kumshukuru kwa kukufanya ufarijike? Naamini Mungu amekujaalia kuwa na mpenzi mzuri, mwenye kila sifa ambayo ulitamani awe nayo, je ulishawahi kumsifia hata kwa kumwambia ni mzuri?
Huenda ulishawahi kufanya hivyo lakini kwa taarifa yako wapo ambao wanahisi kufanya hivyo eti ni ulimbukeni. Ulimbukeni? Kumsifia mpenzi wako  unaona ni ulimbukeni wakati wataalam wa masuala ya mapenzi wanaeleza kuwa, wanawake ni watu wanaopenda kusifiwa sana hata kwa madogo wanayoyafanya?
Unaona hatari gani kumsifia mpenzi wako kuwa ni mzuri? Unadhani unatumia nguvu gani kumsifia mpenzi wako kutokana na mahaba mazito anayokupata? 
Kwa taarifa yako unaweza kuona ni kitu kidogo sana  lakini madhara yake kwenye penzi ni makubwa.
Kumsifia mpenzi wako kwa yale anayokufanyia kuna faida nyingi sana lakini kwa leo nitagusia chache. Kwanza kunaongeza mapenzi. Mume/mke anaposifiwa kuwa anajua mapenzi hata kama si kwa kiwango kikubwa, anafarijika sana.
Unapomwambia mpenzi wako: ‘Dear nashukuru kwa mapenzi uliyonipa jana, umenipa furaha ya ajabu ambayo siamini kama kuna mtu mwingine wa kunipa, nakupenda sana’. 
Maneno kama haya hutumii nguvu wala muda mwingi kuyafikisha kwa mpenzi wako lakini uzito wake ni mkubwa. Kwanza anajihisi aliyekamilika kwa kufikia hatua ya kufanya mambo yakamridhisha mpenzi wake na kwa mazingira hayo anaamini huwezi kumsaliti. Hisia hizo zitamfanya azidi kukupenda.
Hilo ni kwa wote yaani kwa mwanaume na mwanamke. Lakini pia unapomsifia mpenzi wako kwa yale anayokufanyia, unamfanya aongeze kasi ya kukufanyia ili nawe uzidi kumpenda. 
Kwa mfano, unapokutana na mpenzi wako kisha ukamwambia ‘umependeza kweli mpenzi wangu, nazidi kukupenda kwa unavyovaa’. 
Mtu anayeambiwa maneno haya atajitahidi sana siku zote aonekane nadhifu na wa kuvutia kwa mpenzi wake akijua kwamba, akivaa ilimradi kuvaa, hatamfurahisha mpenzi wake. Kwa maana hiyo kumsifia mpenzi wako kunamfanya azidi kuwa bora.
Lakini kusifia kusiwe kwa kinafiki. Usimsifie mpenzi wako eti ili kumfanya ajione bora kumbe katika uhalisia siyo hivyo.
Tusifiane pale inapobidi huku tukijua kuwa kwa kufanya hivyo tutapata faida. Tusiwe na tabia ya kuchukulia poa kila tunachofanyiwa na wapenzi wetu. 
Kama kakuridhisha kimapenzi, msifie kwamba yeye ni muhimu kwako kwa kuwa amekupa ulichotarajia. Amekupikia chakula kizuri, msifie kuwa yeye ni mpishi mzuri. Hiyo italinogesha penzi na utashangaa kila siku inayokwenda kwa Mungu penzi lenu linachanua.
Lakini mbali na hayo, unatakiwa kuridhika kwa kile unachokipata kutoka kwa huyo mpenzi wako ulinaye kwa sasa. Najua kwenye uhusiano wengi tumetoka mbali. Wapo waliowahi kuwa na wapenzi zaidi ya mmoja huko nyuma na kila mmoja alikuwa na kiwango chake cha kukuridhisha. 
Inawezekana kuna ambaye unamkumbuka kwa mapenzi mazito aliyokuwa anakupa zaidi ya huyo uliyenaye. Hiyo ni historia, imepita! Kama huyo uliyenaye si mtaalam sana wa kukufikisha pale unapopata, ridhika na hicho kidogo unachokipata endapo atakuwa anaonesha kukupenda kwa dhati.
Mpe moyo, msifiesifie kidogo kwa hiyo furaha kiduchu anayokupa huku ukiamini kuwa, atabadilika kadiri siku zinavyokwenda.
Kumbuka cha msingi katika maisha yetu ni kumpata mtu mwenye mapenzi ya kweli na si kumpata anayeweza kukuridhisha katika mambo kadha wa kadha.

SABABU ZA WAPENZI KUCHOKANA.

UNAWEZA KUDHIBITI KUCHOKANA?
Ndiyo! Inawezekana kabisa. Ni kweli wapo wengi ambao hujikuta tu wamewachoka wapenzi wao. Pengine hawataki hali hiyo na wanajitahidi kushindana nayo sana, lakini wanashindwa.
Si kwa kutaka ni kwa vile hawajui kitu cha kufanya. Hapa kwenye All About Love nitakusaidia cha kufanya. Twende sasa...
KUOGA PAMOJA
Wanandoa kuoga pamoja ni tendo linaloleta msisimko wa aina yake. Mara nyingi, ndoa inapokuwa changa kabisa, wengi huwa na mazoea haya, lakini wakishazoeana na ratiba kubadilika hili husahaulika.
Utakuta baba anarudi usiku sana, ameutwika vya kutosha, mke amejichokea, kaamua kuoga mwenyewe na baadaye amekula. Anamsubiri mume. Akifika anaingia bafuni peke yake, anarudi chumbani wanalala, asubuhi mchaka mchaka wa kwenda kazini, zoezi hilo haliwezi kufanyika tena.
Ikumbukwe kwamba, kwa kuoga pamoja huzidisha msisimko wa mapenzi na si ajabu hisia za mapenzi zikaamka kwa kasi ya ajabu na baadaye mambo yakaendelea vizuri chumbani. Kwa kuacha kuoga pamoja hupunguza msisimko na ndiyo mwanzo wa kuzoeana na kuchokana.
Ni vigumu sana kuanzisha suala la mapenzi chumbani kwa ghafla tu...huanzia mbali, ikiwemo wakati wa kuoga pamoja. Bila shaka nimeeleweka marafiki zangu. Angalia kipengele kinachofuata...
KULA PAMOJA
Silaha kubwa ya kutochokana ni kufanya mambo mengi kwa pamoja. Inaeleweka kwamba, majukumu ya kila siku husababisha watu kuwa mbalimbali kwa muda mrefu hasa nyakati za mchana, lakini angalau mkipata muda wa kula pamoja, mtakuwa karibu.
Mtasogezana karibu kihisia. Hata kama mnafanya kazi ofisi tofauti, mnaweza kupanga ratiba angalau mara moja kwa wiki, mkatoka mchana na kupata chakula pamoja. Muhimu zaidi ni usiku, wakati wa chakula cha jioni ni vyema wanandoa wakapata muda wa kula pamoja.
Kukaa meza moja huongeza msisimko, utani kidogo tu mtakaofanyiana au kulishana, unaweza kujenga kitu kikubwa na kila mmoja akabaki akimuona mwenzake mpya kila siku.
BUSU
Mwaaa! Tendo dogo sana lakini lenye msisimko wa kipekee. Jenga mazingira ya kumbusu mpenzi wako kila mara. Usikubali kumuacha hivi hivi, hasa kabla ya kulala, kuamka na kuagana naye.
Mbusu shavuni, halafu mwambie: “Nakupenda sana.” Wengi (hasa wanawake) husisimka sana wanapobusiwa shavuni au shingoni. Jizoeshe mtindo huu na kamwe hutajikuta ukimchoka mpenzi wako.
Busu ni alama kubwa ambayo unaweza kumuacha nayo akiikumbuka siku nzima. Atakuchokaje?
KUKUMBATIANA
Tendo hili huambatana na busu. Unaweza kuona ni mambo ya Kizungu sana, lakini hata mnapokuwa peke yenu sehemu ambayo hamuonekani unaweza kumkumbatia mwenzako na kumuongezea msisimko wa kuwa na wewe.
Siku za mwanzo za ndoa, wengi hulala wakiwa wamekumbatiana lakini baadaye tabia hii hupotea ghafla. Hili ni tatizo. Mkumbatie mpenzi wako usiku. Wanawake wengi hulala usingizi mzuri zaidi wanapolala juu ya vifua vya wanaume zao. Kwanini usiwe wewe?
Msogeze karibu yako, mbembeleze ajilaze juu ya kifua chako akideka. Kiukweli utafurahia mapenzi na utajikuta unaendelea kumpa mpenzi wako nafasi ya kwanza kila siku.

Wednesday, 10 December 2014

NDOA NA MSINGI WAKE MKUU.

  Ndoa yoyote ambayo mke au mume hafiki kilele cha Mlima Kilimanjaro..hiyo sio ndoa inayokwenda sawa na kuna madhara makubwa kwa pande zote,kwa maana ya mwingine kuweza kuamua kutoka.Ni vizuri walio kwenye ndoa  kujifunza namna ya kupeana raha iwapasayo wanandoa kuipata.Kama unafikiri mkeo unaye kwa sababu amekuja kutafuta kula au kununuliwa magari na nguo,hilo ni kosa.Tafakari namna ya kupeana raha kwa kila kona.
Kama ni kula,kila mtu anaweza kujitafutia kwa njia mbalimbali.Mwanamke yuko kwa mume kwa sababu anahitaji kupata vitu anbavyo wanawake huvipata kutoka kwa wanaume;Mume ndiyo kichwa,iongoze ndoa yako vizuri kwa hekima.
     Kwa asili,inatakiwa mke na mume kufanikisha zoezi hilo la kuwezeshana kufika kileleni na ni jambo  muhimu kama ilivyo kutoka jasho mwilini,maana sio tu mwili unaondoa uchafu ndani ya mwili,pia inasaidia kuupoza mwili kuwa sawasawa.
Najua wapo wanaoweza kusema aah mbona mimi nimekaa mwaka sitaki tena mwanaume au mwanamke na sijapata madhara...Inawezekana ni kweli,lakini wengi hupata madhara.Kadhalika kuna wengine wanafanya vitu vya hatari kama kutumia vitu mbalimbali kama mwanasesere (sex toys) na mashine maalumu zenye umbo kama la mwanaume au wengine kujichua au kusagana.
Ukidumu bila tendo la ndoa muda mrefu,baadhi ya madhara madogo madogo ni kama kuwa na hasira za mara kwa mara katika mambo madogo,hii hasa kwa wanawake ambao walishawahi kuwa na uhusiano unaokaribiana kuoana au waliwahi kuwa kwenye ndoa kisha wakatoka.
Kwa wanaume madhara yake ni kupendelea zaidi kuangalia picha za ngono.Kwa wote kwa maana ya wanawake na wanaume huwa na hali ya kusahausahau.
  Kwa wanawake wapo ambao hutokwa damu nyingi wakati wa hedhi.Kwa wote yaani wanaume na wanawake hupenda kurukia mambo ya watu wengine ( Tabia ya kufuatilia mambo yasiyokuhusu) na wakati mwingine huongea kwa sauti ya juu hasa kunapotokea migogoro.Wengine wana uwezo mkubwa wa kutukana au kutoa kauli yoyote  unapomuuzi.
Athari nyingine ni kuumwa na kichwa kwa wanaume na wanawake,kupoteza umakini katika kazi na kwa jumla sehemu za kazi wengi wa watu ambao wamesema hawataki tena kusikia mapenzi,siyo viongozi wazuri,wana kauli chafu,hata uamuzi wao mara nyingi siyo mzuri,Ingawa siyo wote.
Hali kadhalika siku ukikutana kimwili na mwenye virusi bila kinga utaambukizwa kirahisi mno.Aidha unaweza kuanzisha tabia nyingine kama ulevi,kukaa ofisini tu bila sababu.
Ni jambo la msingi sana kutafakari kwa umakini mkubwa hali ya uhusiano wako,kwani maisha bila kujipa muda wa kutafakari ni kosa kubwa.Kama ilivyo kawaida ya watu wa biashara ambao hufanya mahesabu ili kuangalia hali za biashara zao,muhimu sana kuangalia mbinu za kufanya ili kama kuna tatizo kwenye uhusiano wako kurekebisha kasoro hizo.
  Ndoa au uhusiano  ambao watu wake hawana muda wa kujitafakari ni vigumu sana kuwa nauhusiano mzuri.
Msingi wa kuwa na maisha bora ni pamoja na kuhakikisha ndani ya ndoa yako kunakuwa na amani thabiti.Unaweza kuwa na fedha kadri unavyoweza,lakini fedha hizo haziwezi kukupa furaha kama huna ndoa nzuri.

Tuesday, 9 December 2014

JINSI YA KUPATA MAPENZI UNAYOTAKA KATIKA NDOA.

   Mkiwa kwenye uhusiano,ni suala la msingi sana kujua namna ya kufanya ili kupeana raha,kwa sababu hakuna mtu anayeingia kwenye ndoa kusaka mtu wa kumtukana matusi au kumpiga.
Wako wanaume ni madikteta,anamburuza mke kadri anavyotaka,wala hajali hisia zake,kitu ambacho ni kibaya.Kuna wanaume wanafikiri wanawake ni kama gunia,unamfanyia vituko na matusi unavyotaka,unamnyanyasa na kumsema kwa watu kadri unavyotaka,kitu ambacho si sawa,kuna wanaume wengine licha ya kutanbuliwa kama vichwa vya nyumba,akikwaruzana na mwenzi wake,anachokijua ni kununa,kususa au hata kulala sebuleni,hii ni akili ya kitoto.
Mume kama kichwa cha nyumba,kinapaswa kuwa mfano wa kuigwa.Kila mwanaume anapaswa kujiangalia matendo yake.Lakini pia kila mwanamke anapaswa kuangalia  matendo yake anayofanya kwa ndoa yake na kwa mumewe.Je, ni matendo ya haki? Kila mwenye akili timamu anapaswa kufanya vitu ambavyo yeye akifanyiwa,atajihisi kupata raha.
Wakati mwingine tunakuwa na ndoa mbaya kwa sababu ya matendo tunayotenda.Ni lazima uwe makini kwa vitu ambavyo unafanya.Lakini ni muhimu katika uhusiano kuwa na kawaida ya kuwa na muda wa kutafakari kwa umakini mkubwa hali ya ndoa yako na kuona ni yapi yanakwenda hovyo au yanakwenda safi.Katika maisha msingi wa kuwa na maendeleo mema ni kuwaza na kufanya mema,ndio kusena hata kama labda ndoa yako ina matatizo,unapaswa kuwaza namna ya kufanya mema kwa maana ya kuondoa kasoro zilizoko na kadhalika.
Ni ujinga kutarajia mazuri kwenye ndoa yako wakati hufanyi mazuri,Ni  suala lisilowezekana,Utakuta mwanaume au mwanamke ni jeuri,lakini bado anatarajia maisha yake yawe na faraja,kitu kisichowezekana.Ni ujinga kukimbilia mwanamke au mwanaume mwingine na kuiacha ndoa yako,kwa sababu hakuna ambaye hana kasoro.Kama unafikiri yupo mwanamke au mwanaume ambaye hana kasoro,jua kuwa fikra zako haziko sawa.Kwa ufupi ni kwamba katika kila ndoa,kuna wakati kunatokea hitilafu,cha msingi ni kukaa chini na kuondoa kile ambacho kinaleta shida.
Cha msingi ni kwa watu kuacha dharau,kuacha majivuno,kuacha kuona kwamba  aaah nikimuomba msamaha ataona najikomba,hakuna ubaya kuitwa unajikomba ikiwa unachokitaka ni kizuri kwa ndoa yako.