Wednesday, 18 November 2015

MAZOEZI HUONGEZA HAMU.

Tafiti nyingi zinaonesha kwamba kufanya mazoezi ya kawaida huongeza kiwango cha homoni za endorphins ambazo huhusika na kuongeza intensity ya kusisimka kimapenzi.
Ile kujisikia upo fit kimwili hukusaidia kujisikia mzuri zaidi na pia husaidia kukupa mood ukiwa chumbani.
Hata hivyo kuna limit ya mazoezi kwani ukifanya mazoezi magumu zaidi yanayopitiliza kiwango kama vile mkimbiaji wa marathon au kuendesha bicycle kwa muda mrefu (kwa mwanamke husababisha kuwa na clitoral dumbness –kisimi kupoteza uwezo wa kusisimka tena), kwa pamoja haya mazoezi huweza kukufanya uchoke na kushindwa kuwa na hamu ya tendo la ndoa.

Hivyo mazoezi ni muhimu lakini yasiwe ya kuzidisha!

Monday, 9 November 2015

NI RAHISI SANA KUIMARISHA NDOA YAKO.

ILI uwe na ndoa yenye furaha ni lazima utenge muda wa kutafakari namna ya kuiboresha na
kutafuta furaha ya ndoa hiyo. Ndugu zangu, kila kitu kinatengenezwa.

Waswahili wanasema, ukiona vyaelea, ujue vimeundwa. Huwezi kuacha mambo yakajiendesha hovyo ukategemea kuwa na ndoa bora. Uhusiano imara unakutegemea wewe.
Kila mmoja ana wajibu wa kuangalia furaha ya mwenzake. Yapo mambo mengi muhimu ambayo kama
wanandoa wakiyafanya huboresha uhusiano wao, lakini hapa nitakutajia yale muhimu zaidi.

ISHI KIRAFIKI.

Kuna baadhi ya wanandoa wakishaingia kwenye muunganiko huo, ule urafiki uliokuwa zamani wakati wa uchumba, hilo ni tatizo. Ukitaka kuwa na ndoa yenye furaha lazima umfanye mwenzi wako kama rafiki yako.Baadhi ya wanaume wana tatizo la ubabe na kujiona kuwa wao ni wanaume hivyo hawapaswi kuguswa kwa lolote.

Ndoa inageuka jeshini. Hilo ni tatizo.
Mshirikishe mwenzako kwenye mambo yako. Kuwa na kauli njema muda wote. Sikiliza shida za
mwenzako na namna ya kuzitatua.

Sikiliza pia hisia zake.Usipoishi naye kirafiki, maana yake ataogopa hata kukueleza mambo fulani ya msingi ambayo labda havutiki nayo. Ukimsogeza kama rafiki atakueleza mambo ambayo hayamfurahishi.
Mkiishi kama marafiki ni rahisi kusameheana. Ndoa nzuri ni ile yenye kusameheana ndani yake.
Kukaa na mambo moyoni husababisha mikwaruzano ya kudumu.
Kama marafiki, mtapata muda wa kushughulikia kero zenu haraka kabla hazijakua.

MIPANGO YA KIFEDHA.

Kama kuna jambo linalosabisha migongano na kupunguza uaminifu ndani ya ndoa ni suala la
fedha. Kwa bahati mbaya sana wanaume wengi ni wasiri sana kuhusu mapato yao.
Huna sababu ya kumficha mke wako kuhusu kipato chako. Mshirikishe, ajue unapata kiasi gani kwa mwezi. Labda una biashara nyingine au vyanzo mbalimbali vya mapato nje ya ajira yako ya kudumu, zungumza na mwenzako.

Ziko faida nyingi, kwanza ataona unavyomwamini na kumthamini na kumfanya sehemu ya mafanikio
ya familia, lakini pia anaweza kukushauri mambo ya msingi ambayo yatasaidia kukuza kipato
chenu.

Kubwa zaidi ni kwamba, utamfundisha namna ya kuendesha biashara zako, hata siku ikitokea
umeugua atasaidia kuimarisha biashara.

MATATIZO YA FAMILIA
Kuangalia matatizo ya pande zote mbili za familia mlizotoka, inasaidia kuimarisha mapenzi.
Mwenzako akikuambia kuhusu tatizo labda la mtoto wa dada yake, usipuuze.
Hata kama hamna fedha, unaweza kumshauri jambo zuri ambalo litamuweka vizuri kihisia.

Wengine huwa na majibu mabaya: “Kwani nimekuoa wewe au ukoo mzima?” kauli hii siyo sahihi na
hubomoa nyumba.

Kujua na kuthamini matatizo ya mwenzako ni kati ya mambo muhimu sana yanayoleta furaha kwenye ndoa. Kuwa na kauli nzuri. Kweli, inawezekana huna fedha au mipango yenu imeingiliana, isiwe tatizo.

Mjulishe mwenzako kwa lugha laini na ikiwezekana mawazo yako yanaweza kumfanya akajua mahali
pa kuanzia. Kuchukulia tatizo la mwenzako kama lako, inaongeza amani, maana anajiona sehemu
kamilifu ya muunganiko wenu wa ndoa.

Wengi hawajui hili na hata kama wanajua, hawatoi umuhimu mkubwa kwa wenzi wao. Ndoa ni tunu
rafiki zangu. Tujitahidi kuheshimu na kuzilinda kwa nguvu zetu zote.

Friday, 6 November 2015

JINSI GANI UBIZE UNAVYOWEZA KUSABABISHA UPWEKE KWA MWENZI WAKO?

Kuna ndoa ambazo ukizifuatilia zinasikitisha sana. Ni ndoa ambazo furaha imetoweka, yaani kila mmoja yuko kwenye ndoa ili mradi tu yupo lakini hatimizi yale ambayo yanatakiwa kufanywa na mwanandoa.
Upweke ni jambo linaloumiza sana hasa kwa mtu aliye kwenye ndoa.
Mapenzi si pesa, mapenzi si kumvalisha na kumlisha mkeo kila anachokitaka. Mapenzi ni ukaribu wa wewe kwake. Unatakiwa kujua kwamba, mumeo/ mkeo atajisikia faraja sana ukiwa pembeni yake pale atakapokuhitaji.
Ni jambo linaloumiza sana kwa mke kukosa muda wa kuwa na mume wake eti kisa ‘ubize’. ‘Ubize’ huu mpaka lini? Sikatai kuchakarika ndiyo maisha lakini ndiyo iwe kila siku?
Hiyo furaha ya ndoa itapatikana vipi ikiwa wanandoa wenyewe hawapati muda wa kuwa pamoja? Hili ni tatizo na kwa kweli tusipoangalia tunaweza kuwanyong’onyesha wenza wetu bila kujua na mwisho kuwafanya waumie kimoyomoyo.
Lakini cha ajabu ni kwamba, kama ilivyo kwa wanaume, wapo wanawake pia ambao wanajifanya wako bize sana na maisha kuliko kuzijali ndoa zao.
Yaani wao wanakutana na waume zao kwenye tendo la ndoa kwa masharti na tena kwa ratiba. Mapenzi gani haya? Mumeo anataka haki yake unamwambia umechoka! 
Sasa kuna faida gani ya wewe kuolewa? Kama unahisi kazi ni bora kuliko kumjali mumeo, heri uwe muwazi kwake ili aoe mwanamke mwingine atakayejali hisia zake.
Kikubwa ninachotaka kusisitiza kwenye makala haya ni kwamba, kila aliye kwenye ndoa ahakikishe anatenga muda wa kutosha wa kuwa karibu na mwenza wake bila kujali ubize unaotokana na mishemishe za kimaisha.
Hii itaimarisha ndoa na hakika kila mmoja atafurahia uwepo wa mwenzake. Tukumbuke hakuna asiyetaka mwenza wake kujishughulisha kwani maisha bila kuwa bize hayawezi kuwa mazuri lakini sasa ubize huu ukizidi kiasi cha kumfanya mwenza wako akawa mpweke, inakuwa siyo poa.


SIRI MUHIMU UNAZOTAKIWA KUZIJUA KUHUSU WANAWAKE

UKWELI ambao haukwepeki kuhusu uhusiano na mapenzi ni uwepo wa furaha, amani na maelewano. Hivi ni vitu muhimu sana. Msingi wa yote ni pendo la dhati. Ikiwa wapendanao wana upendo wa kweli toka mioyoni mwao ni rahisi kutunza vitu hivyo.
Hakuna asiyependa kuwa na uhusiano wenye furaha na amani. Uhusiano wenye masikilizano huzaa matunda mema – kama ni marafiki tu, basi ujue ndoa inanukia lakini kama tayari ni wanandoa, maana yake mafanikio ndani ya nyumba yatakuwa rahisi kupatikana. katika yote hayo, inategemewa zaidi na namna wahusika wanavyoendesha uhusiano wao; kwa maana kwamba, yote yanahitaji ushirikiano wa wote. Hapo ndipo mwanzo wa matatizo. Wenzi wawili huwa na tofauti za hulka.

Kwa wanawake, wengi hupenda sana kufuatilia na kuhakikisha uhusiano unakuwa imara. Likitokea tatizo, mwanamke huwa mstari wa mbele kulishughulikia ili mambo yaishe. Wanawake wengi hawapendi kuwa wamewaudhi wenzi wao.
Ikitokea wakiona kuna tofauti ya kimawasiliano, mara moja husaka mbinu za kutatua na kubakisha uhusiano ukiwa kwenye hali nzuri. Hiyo ni tofauti na wanaume ambao mara nyingi wao ni watu wa harakaharaka.

Ni wepesi wa kusahau mambo au kuyachukulia kwa wepesi. Mfano, mwanamke wake akikasirishwa na jambo fulani, ni rahisi tu kuishia kusema: samahani. Wakati mwingine anaweza asiseme kabisa, akijua mambo yameshaisha. Wanawake ni tofauti. Wanafanya mambo yao kwa taratibu sana. Hasira zao zinachelewa kuisha, lakini ni rahisi zaidi kuzimaliza kwa kumwambia tu: nakupenda mpenzi, najua nimekosea, samahani mama.

Ni sentesi fupi sana lakini kwao ina maana na thamani kubwa sana. Mapenzi ni sawa na bustani, wakati mwingine inahitaji kumwagiliwa na kuwekewa mbolea. Kama ni kweli unampenda, tuliza akili na muda wako kuhakikisha furaha yake inaendelea kuwepo.

Inamaanisha kuwa, upendo wake kwako ukitamalaki muda wote – mafanikio ya kazi ya mikono yako yapo jirani tu. Mfanye mwanamke wako atabasamu. Pamoja na ubize wako, tenga nafasi kidogo kwa ajili yake.

MSAMAHA SI KUJISHUSHA!

Wanaume wengi wanaamini kumwambia mwanamke samahani ni kujishusha na kuwa chini yake, si hisia sahihi. Msamaha ni uungwana. Kama kweli unampenda kwa dhati, una shaka gani kumwambia akusamehe ili uhusiano uendelee kuwa wenye nguvu?

Hutapungua mahali popote kukubali kosa, ikiwa umekosea au kumrekebisha mwenzako badala ya kubaki bubu huku ukiwa umenuna na kusitisha baadhi ya huduma. Kama ilivyo kwako, tambua kuwa mwanamke naye ni binadamu, anaweza kufanya makosa lakini asijue!

Kumwambia kwa upole ni jambo zuri. Atakusikiliza, atakuelewa na atajirekebisha alipokosea. Kukaa nalo moyoni hakuna maana.

PUNGUZA UBABE.

Wapo baadhi ya marafiki wanaamini kuwa ubabe ni sehemu ya ukamilifu wa uanaume. Siyo kweli. Huna sababu ya kuwa mkali sana au mwenye amri muda wote. Mwanamke anahitaji kubembelezwa, upendo na kuonyeshwa namna anavyothaminiwa.

Wengine wana tabia ya kuwapiga wenzi wao, kitu kidogo tu, tayari kipigo. Vipi akikutana na mkarimu, asiyepiga na anayebembeleza? Akiachana na wewe utamlaumu nani? Ni kweli kuna wakati mwanamke anahitajika kukaripiwa akikosea, lakini si sawa kuwa mkali kupitiliza wakati wote.

Tuesday, 3 November 2015

WALIO NJE WANALAZIMISHA NDOA,WALIO NDANI WANADAI TALAKA.

NDOA inafahamika kuwa ni heshima kwa kila mmoja, namaanisha kwa anayeoa na anayeolewa. Mwanaume akioa, anaheshimika na anajiona ameingia kwenye majukumu ambayo yanamlazimu atie akili ili aweze kukabiliana nayo.
Kwa wanawake ndiyo usiseme. Yaani idadi kubwa ya wanawake wanalilia ndoa hasa kwa wanaume ambao wamewapenda na kuwaamini kwamba wakiwa nao ndani maisha yao yatakuwa ni ya furaha zaidi.
Kwa kifupi ndoa ni tamu ila kama utaijulia na ni chungu kama utakuwa umeingia kwenye maisha hayo na mtu ambaye awali alikuwa akijifanya anakupenda sana lakini baadaye akaamua kutoa makucha yake.
Wapo wanaume ambao leo hii wanalia, wanajuta ni kwa nini waliamua kuwaoa wanawake ambao wamewaoa. Wanajuta kwa kuwa wanakutana na mambo ya ajabu ambayo hawakuyatarajia.
Si hivyo tu, wapo wanawake ambao walifurahi walipovishwa pete za uchumba na hatimaye kuvaa mashela lakini leo hii wanaomba talaka kutoka kwa waume zao kutokana na mazingira tofauti wanayokumbana nayo.
Kwa kifupi baadhi ya walio kwenye ndoa wanalia, unaweza kuwaona wakipita mbele za watu wanachekacheka na kuonesha kuwa wanapendana lakini kumbe katika uhalisia, wamechokana na ndoa zao zimeshikiliwa na nyuzi.
Unaweza kujiuliza ni kwa sababu gani? Inakuwaje watu waliotokea kupendana sana wanaishi kwa muda mfupi tu kisha wanaanza kujutia maamuzi yao ya kuingia kwenye ndoa?  
Hakuna sababu nyingine zaidi ya kwamba aidha walikurupuka kufanya maamuzi hayo au kulikuwa na mazingira ya mmoja kujifanyisha na kumfanya mwenzake aone amempata mtu sahihi kumbe hamna kitu.
Ukijaribu kuchunguza sana, utabaini kuwa wengi wako kwenye ndoa za Kichina. Ndoa ambazo hakuna mapenzi ya dhati baina yao na kusalitiana imekuwa ndiyo mtindo wa kisasa. Katika mazingira haya furaha haiwezi kupatikana na ni lazima majuto yatokee.
Ni kwamba, ndoa kweli ni heshima na kama umetokea kuwa kwenye uhusiano na mtu ambaye unaona ana kila kigezo cha kuwa mwenza wako, una kila sababu ya kufanya kila uwezalo kukaribisha ndoa. Oa au olewa ili furaha yako iweze kukamilika.
Lakini sasa angalizo ni kwamba, si kila anayeonesha kukupenda sasa anafaa kuwa mumeo au mkeo. Elewa kwamba kuna wanawake wengine ambao wao kupenda kwao hawamaanishi ni ili waolewe, wanapenda tu na kufurahia kampani lakini ukiwatajia ndoa, usije ukashangaa wakakataa kuolewa. Hawa wa sampuli hii ukiwalizimisha utakiona cha mtemakuni.
Namaanisha kwamba, wapo wanawake ambao lile neno ndoa tu kwao limewakalia kushoto lakini wanajua kupenda na kuwaridhisha wanaume. Ni sawa na kulazimisha kumuoa changudoa ambaye ni mtaalamu wa kudatisha, mtaalamu wa kubembeleza na mtaalamu wa kumpa furaha mwanaume yeyote kwa kuwa ameona pesa.
Ukimuoa mwanamke wa aina hiyo ukidhani utapata mambo kama hayohayo,umeumia. Hilo lipo pia kwa wanaume, kuna wale ambao wanaweza kuonesha upendo wa hali ya juu lakini hawako tayari kuingia kwenye ndoa. Ukilazimisha kuolewa na mwanaume huyo, umeula wa chuya kwani huwezi kuyapata mapenzi aliyokuwa akikupa kabla ya ndoa.
Kwa maana hiyo nihitimishe kwa kusema kuwa, lazimisha ndoa lakini kwa mtu ambaye una uhakika anahitaji kuingia kwenye ndoa na umemsoma vizuri na kubaini hawezi kuja kukuletea maumivu siku za baadae.

Thursday, 22 October 2015

HAYA NI MUHIMU BAADA YA KUMALIZA TENDO LA NDOA.

Labda kwa wale wasiofahamu niwaambie tu kwamba dhana ya mapenzi ni dhana yenye wigo mpana sana na ndiyo maana hutasikia hata siku moja tumepumzika kuizungumzia.
 
Hata hivyo, tunachofanya siku zote ni kukumbushana kwa yale tunayoyafahamu na kushauriana kwa pale tunapohisi wengi hufanya makosa.
 
Baada ya kusema hayo sasa nigeukie mada yangu ya leo ambayo kwa kiasi kikubwa inawahusu wale walio kwenye ndoa na kikubwa nazungumzia yale ambayo wawili waliotokea kupendana kwa dhati wanatakiwa kuyafanya mara baada ya kumaliza kufanya tendo la ndoa.

Wengi wamekuwa wakifanya makosa na kujikuta wakishamaliza kufanya tendo hilo takatifu, kila mmoja anageukia kwake kisha kuuchapa usingizi.
 
Sisemi kwamba ni lazima kuyafanya haya nitakayoyaeleza leo ila 
yakifanywa huwa na manufaa yake na mara nyingi yanaboresha uhusiano.
 
1.KUOGA PAMOJA.

Mtakuwa ni watu wa ajabu kama mtamaliza kufanya tendo hilo kisha kila mmoja kulala na majasho yake. Wapowasiojali katika hili na kuona kuoga au kutooga ni uamuzi wa mtu. Elewa linapokuja suala la usafi inashauriwa mkimaliza lazima muoge.
 
Wapo wanawake ambao wakishamaliza hukimbilia kuwaandalia maji wenza wao, wakishaoga ndipo nawo huenda kuoga. Hivi unaona ugumu gani kwenda kuoga na mwenza wako? Unaijua raha ya kuoga na huyo wako wa maisha?
 
Wanaofanya hivyo wanajua raha yake na wewe ambaye hujawahi, anza leo. Mmemaliza mambo yenu, chukuaneni kimahaba, elekeeni bafuni kisha ogeshaneni kimahaba.
Baada ya hapo rudini chumbani, mkishajifuta maji pandeni kitandani mkiwa wapesi.
 
2.KUSIFIANA.

Hakuna muda maalum uliotengwa kwa ajili ya wanandoa kusifiana. Hilo linaweza kufanyika wakati wowote lakini pale mnapomaliza kufanya tendo la ndoa ni lazima utakuwa na jambo zuri la kumuambia mwenza wako.
Msifie kwa utundu na ubunifu wake. Msifie pia kwa mapenzi matamu anayokupa na ikibidi mpe sifa ya uzuri wake kiasi cha kukufanya kila unapokuwa karibu yake ujisikie amani ya kupitiliza.
Wapo ambao hawana kabisa kasumba ya kuwasifia wala kuwashukuru wenza wao kwa mazuri wanayofanyiwa. Yaani wao wanachukulia kila kitu poa tu bila kujali kwamba kusifiana kunanogesha mambo.
 
3.KUELEKEZANA.

Kwenye kale kamchezo, wapo ambao wanakosea, kuelekezana na kukosoana kwa wapenzi ni jambo la kawaida. Yawezekana mwenza wako alifanya kitu ambacho hakikukufurahisha wakati mkiendelea na burudani yenu, mnapomaliza mwambie lakini kwa lugha ya kimahaba na ya upole. Naamini kwa kufanya hivyo atakuelewa na kubadilika

4.ZUNGUMZIENI MAISHA.

Huu ni wakati muafaka wa kujadili changamoto na malengo katika maisha yenu. Hapa akili zinakuwa zimetulia na kila mmoja anakuwa na mawazo chanya kwa mwenza wake. Jadilini mambo yenu, wekeni mikakati ya kuliboresha penzi na maisha yenu kwa ujumla.
 
Hayo ni baadhi ya mambo ambayo mnashauriwa kuyafanya pale mnapomaliza kufanya tendo la ndoa.
 

Friday, 16 October 2015

BADO MAPENZI YANAKUTESA?..1

Ni wazi kwamba mapenzi yanachukua nafasi kubwa sana katika maisha ya binadamu, na ipo dhahiri kwamba mapenzi yanaweza kuleta furaha maishani mwako lakini wakati huohuo yanaweza kuleta maumivu, mateso na karaha.

Watu wengi sana bado wanalizwa na mapenzi na hii ni kwa sababu hawafuati kanuni sahihi ya mapenzi, ndiyo, mapenzi yana kanuni zake.

Kwa bahati mbaya kabisa, kwa sasa mapenzi yamegeuzwa na kuwa kama kitu cha kujaribu au kufanyia biashara na ndiyo maana yanawatesa wengi. Lakini ni kwanini mapenzi  yaendelee kututesa?  au ni kwa sababu hatujui maana halisi ya mapenzi.

MAPENZI NI NINI?
Katika hali ya kawaida, mapenzi hayaelezeki kuwa ni nini. Ni vigumu sana mtu kukueleza maana ya mapenzi ndiyo maana kila mtu ana uelewa tofauti juu ya suala hilo.

Mtaalamu mmoja wa masuala ya mapenzi aliwahi kuyaelezea mapenzi ndani ya kitabu chake cha More About Love, ambapo alisema; ‘Love is natural feelings, which take place from the deepest part of your heart upon somebody or something else’ akimaanisha kuwa mapenzi ni hisia za asili ambazo huchukua nafasi kutoka sehemu ya ndani kabisa ya moyo juu ya mtu au kitu chochote. Tena bila kuwa na visingizio au masharti ya aina yoyote.

HISIA NI NINI?
Huu  ni msukumo wa vichochezi katika homoni za  ndani ya mwili ambazo hutokea kutokana na  mazingira husika.
Lakini huwa tofauti kati ya mtu na mtu na ndiyo maana watu hutofautiana madaraja ya kupenda.

Mfano halisi ni kwamba, utakuta mtu anapenda sana wanawake weupe, lakini mwingine hataki hata kuwaona.
 Lakini mapenzi siyo mawazo au uamuzi wa mtu, bali mapenzi ni hisia ambazo hutokea pasipo uamuzi wa mtu.

Kutokana na hali hiyo, utasikia mtu akisema ‘sijui nimempendea nini huyu mwanaume’ ni kweli yeye hajaamua lakini hisia zimefanya awe hivyo.

USIRUHUSU  MAPENZI YAKUTESE
Kwa nini mapenzi yakuumize? Unakosea wapi, kwanini ukataliwe kila mara? Haya ni baadhi ya maswali ya kujiuliza kuhusu mateso ya mapenzi.

Kamwe katika maisha yako usiruhusu mapenzi yakutese, najua yawezekana kila mpenzi unayempata haudumu naye, wewe ni mtu wa kulia kila siku, hujawahi kufurahia maisha hataa siku moja, jipange upya.

Thamini na jali zaidi maisha yako kwanza, fikiria kipi ni bora kati ya mapenzi na maisha yako, ni kipi kilitangulia? Kama maisha ndiyo yalitangulia  kwa nini usijijenge kwanza kimaisha ndipo mengine yafuate?

Hata kama unateswa na mtu unayempenda kwa dhati, hata kama ni mzuri kushinda malaika, kwani bila yeye maisha hayaendi? Si kweli na kama unaweza kuishi bila yeye kwa nini akutese namna hiyo?

Hakuna kitu kinachouma kama mapenzi endapo utakosea kanauni zake, ukaruhusu moyo wote kuelekea huko, hakika yatakutesa.

Itaendelea....